1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa waasi Nigeria, adai kutotenda kosa lolote

20 Januari 2022

Kiongozi wa kundi la wanaotaka kujitenga nchini Nigeria amekanusha kuwa na hatia ya mashtaka zaidi katika kesi yake ya ugaidi jana, miezi sita baada ya kukamatwa nje ya nchi na kurejeshwa nchini humo.

https://p.dw.com/p/45pEZ
Karte Nigeria Biafra
Picha: DW

Nnamdi Kanu, kiongozi wa vuguvugu lililopigwa marufuku la Indegenous People of Biafra, IPOB ambalo linataka taifa tofauti la watu wa kabila la Igbo kusini-mashariki mwa Nigeria alikuwa tayari anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uhaini.

Lakini waendesha mashtaka katika mahakama ya Abuja waliongeza mashtaka mengine nane katika kesi yake ikiwemo uchochezi wa vurugu kabla ya kufikishwa kwake mahakamani hapo wiki hii, kulingana na timu yake ya mawakili.

Kanu amekana mashtaka hayo yote na mawakili wake wamewasilisha ombi la kufutwa kwa mashtaka yote, ambako kikao kingine cha kusikiliza hoja kimepangwa tarehe 16 Februari.

Tizama Picha: 

Kanu alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Mwezi Juni mwaka jana, mwanasheria mkuu Abubakar Malami alitangaza kwamba Kanu allirejeshwa nchini Nigeria ili kukabiliwa na mashitaka yanayomkabili.

Maafisa hata hivyo hawakueleza mahali alipokamatwa Kanuna namna walivyomkamata. Lakini familia na wanasheria wake wamesema alikamatwa kinyemela nchini Kenya na kurejeshwa Nigeria.

Miito ya uhuru ama kujitenga huwa ni tete mno kusinimashariki mwa Nigeria, ambako vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takriban miongo mitano iliyopita vilisababisha karibu watu milioni moja kufariki dunia kutokana na mapigano na hata njaa.