1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KILABU YA KABUMBU DORTMUND YAKABILIWA NA MUFLIS

AHMED M SALEH18 Februari 2005

Burussia Dortmund, ikiwa miongoni mwa vilabu mashuhuiri kabisa vya kabumbu barani Ulaya na kimataifa imekabiliwa na kitisho cha kwenda muflis. Ikiwa ni mwanachama wa soko la hisa, kilabu hiyo inaweza tu kunusuriwa ikiwa wafadhili wake watakubalia mpango wa kupatiwa kilabu hiyo muundo mpya kabisa wa kuendesha harakati zake za kibiashara, alisema mkuu wake Michael Meier hapo jana. Pindi ukishindwa mpango huo basi haina budi kutangazwa muflis Borussia Dortmund, bingwa wa mara sita wa Ligi ya Kabumbu ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHZQ

Miaka minne kutoka sasa mji wa Dortmund una mipango ya kusherehekea miaka 100 tangu kuundwa kilabu ya Borussia Dortmund. Kilabu imepanga kusherehekea pamoja na washabiki wake wanaokaribia kuiabudu Borussia. Tatizo moja kubwa ni kuwa hadi wakati huo huenda pasiweko tena kilabu ya Borussia Dortmund ambayo iliyowahi kushinda hata kombe la Ulaya na kombe la dunia la kabumbu, iko njiani kwenda muflis. Mustakabali wa kilabu hiyo haumo tena katika himaya ya wachezaji wake kumi na moja uwanjani, bali umo katika mikono ya wafadhili wake. Na pindi mmoja tu wa wafadhili hao ataikatalia mikopo mipya basi huo utakuwa mwisho wa kilabu yenye jazi mashuhuri za manjao kwa nyeusi, na shirika la kabumbu la Ujerumani kukabiliwa na kashfa mpya ambayo haipendezi kabisa mwaka mmoja kabla ya kufanyika kombe la dunia katika nchini humu. Hata bado haijapoa ile kashfa ya ulaji rushwa ya mwamuzi kabumbu wa Kijerumani, sasa Burussia inakabiliwa na kitisho cha kuteketea, kilabu ambayo ni shida kuwaza kuwa haimo tena katika Ligi ya Ujerumani, ambayo kama inavyoonyesha mnamo miaka ya nyuma imefamnya kila kitu kinyume cha ada.

Na litakuwa kosa kusema kuwa tatizo linatokana na uamuzi wake wa kujiunga na soko la hisa miaka minne iliyopita. Kwa hakika hiyo ilikuwa hatua ya kishujaa wakati Borussia ilipokuwa katika kilele cha mafanikio yake, hatua ambayo ingechukuliwa na kilabu yoyote mashuhuri ya kimataifa, Manchester United ikiwa ni mfano mzuri kabisa wa kilabu iliyofanikiwa sana katika soko la hisa. Swali kubwa ni: ikiwa Borussia inataka kufanikiwa kama Manchester, kwa nini hawakuiendesha kilabui yao kistadi kama Waingereza? Ukweli ni kuwa asili miya 80 ya mapato ya kibiashara ya Borussia zimetumiwa ovyo, jambo linalowakereketa sana washabiki wake wengi walioweka rasil mali zao katika ununuzi wa hisa za kilabu. Wala haikusaidia kitu kuwa kilabu ilijaribu kuwatuliza washabiki wake. Sababu ziko wazi kabisa. Borussia Dortmund ni mojawapo ya vilabu vilivyotumia pesa nyingi kupita mpaka katika ununuzi wa wachezaji mashuhuri, pamoja na kuwa umekarabatiwa sivyo kabisa ujenzi wa kiwanja chake kipya, zikiwa harakati za pumbavu za kibiashara zitakazomshangaza bingwa yeyote wa kiuchumi. Na wakati Borussia ikiendelea kupata ushindi katika viwanja vya kabumbu mameneja wake walikuwa wakizitosa pesa kwa miliyoni katika miradi isiyokuwa na miguu wala kichwa. Na kila walipopandisha matumizi, waliiongezea kilabu kitisho cha kwenda muflis. Ikafika hadi ya kuanza mtindo mbaya wa kuongeza mikopo na kutathminiwa upya nguvu zake za kibiashara. Na mabingwa wa kunusuru muflis hawakuwa na njia yoyote nyingine isipokuwa kuzinyakua pesa za viingilio vya watazamaji na hata kuliuza kisiri jina mashuhuri la kilabu hadi kuwa sasa inajikuta msingini. Ni swali jengine iwapo katika hali yake ya sasa Borussia inaweza kunusurika. Na wamekosea wale wanaoshutumu sasa kuwa vilabu vya kabumbu havifai kujiunga na masoko ya hisa, kwa sababu zaidi ya nusu ya vilabu vya kabumbu barani Ulaya vimefanikiwa katika masoko ya hisa. Lakini ukweli mwengine ni kuwa vilabu vya Kijerumani havifai kujiunga na masoko ya hisa, kwa sababu havina muundo muwafaka wa kuchuana na mashindano yake.