1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Kiev yashambuliwa kwa makombora ya Urusi

19 Desemba 2022

Mashambulizi ya makombora ya Urusi yameushambulia mji wa Kiev mapema Jumatatu, siku moja baada ya mji huo mkuu wa Ukraine kugubikwa na mashambulizi mabaya ya makombora tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Februari 24.

https://p.dw.com/p/4L9in
Ukraine Krieg | Angriff auf Kiew
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Utawala wa kijeshi wa mji wa Kiev umesema kupitia mtandao wa kijamii kuwa ving’ora vya tahadhari vilisikika mara 23 na kwamba kikosi cha anga kimezidungua ndege 18 zisizo na rubani kwa kutumia mifumo ya ulinzi ya Ukraine. Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa vikosi vya Urusi vilikuwa vinatumia silaha aina ya Shahed zilizotengenezwa nchini Iran.

Mkaazi mmoja wa Kiev, Anatoly anaelezea jinsi mashambulizi hayo yalivyotokea. ''Mlio ulikuwa kama tetemeko. Nilikuwa upande wa pili. Ghafla nilisikia kelele na mara mripuko mkubwa. Mripuko wa kwanza. Kisha dakika tatu hadi nne baadae, nikasikia mripuko wa pili,'' alifafanua Anatoly.

Meya wa mji wa Kiev Vitali Klitschko, amethibitisha kwamba mashambulizi yametokea kwenye wilaya za Shebchenkivskyi na Solomianskyi zilizoko magharibi mwa Kiev. Kwa mujibu wa Klitschko, miundombinu muhimu imeharibiwa, lakini hakuna vifo vilivyotokana na mashambulizi hayo.

Vitali Klitschko
Meya wa mji wa Kiev, Vitali KlitschkoPicha: John Moore/Getty Images

Kampuni ya nishati ya Ukraine, DTEK imesema mashambulizi hayo yatasababisha umeme kukatwa kwa dharura kwenye mji huo. Ufaransa na Umoja wa Ulaya zimesema mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya raia ni sawa na uhalifu wa kivita, huku mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Josep Borell akiyaita mashambulizi hayo kuwa ya "kinyama".

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema kufikia jana jioni, watu milioni tisa walirejeshewa umeme. Baada ya mashambulizi makubwa kutokea kwenye miji mingi iliyohusisha zaidi ya makombora 70 siku ya Ijumaa, shirika la umeme la Ukraine lililazimika kukata umeme kwa dharura wakati likifanya juhudi za kukarabati gridi ya umeme iliyoharibiwa.

Hali ya mpakani kipaumbele cha Ukraine

Katika hotuba yake ya usiku, Zelensky alisema pia hali katika mpaka wa Ukraine na Urusi na Belarus ni kipaumbele cha mara kwa mara na kuwa wanajiandaa kwa hali yoyote inayowezekana ya kiulinzi, na kwamba suala la mpaka lilijadiliwa katika kikao na makamanda wake wa kijeshi.

Matamshi hayo ameyatoa wakati ambapo Rais wa Urusi Vladimir Putin, anasafiri kwenda Belarus. Katika nchi hiyo jirani na Ukraine kwa upande wa mpaka wa kaskazini, wanajeshi wapatao 9,000 wa Urusi wamewekwa huko kama sehemu ya kikosi cha kikanda wakijianda kwa luteka ya kijeshi.

Russland | Treffen Präsident Alexander Lukaschenko und Wladimir Putin
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko na Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Ramil Sitdikov/POOL/TASS/dpa/picture alliance

Shirika la Habari la Interfax limeripoti kuwa luteka hiyo inafanyika Jumatatu wakati Putin anaizuru Belarus ambapo atakutana na Rais Alexander Lukashenko ambaye ni mshirika wake muhimu kwenye mji wa Minsk. Hii ni ziara ya kwanza ya Putin nchini Belarus katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hofu ya Urusi kupeleka wanajeshi wake Belarus

Kupelekwa kwa majeshi ya Urusi nchini Belarus kulizusha hofu kwamba wanajeshi wa Belarus wanaweza kuungana nao katika uvamizi wao Ukraine.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak siku ya Jumatatu anatarajiwa kutangaza msaada mpya wa silaha kwa Ukraine, katika mkutano na viongozi wenzake wa mataifa ya Nordic, Baltic na Uholanzi kwenye mji mkuu wa Latvia, Riga.

Uingereza inatarajia kuipatia Ukraine maelfu ya silaha za kivita zenye thamani ya dola milioni 304 chini ya mkataba ambao utahakikisha upelekwaji wa mara kwa mara wa silaha katika mwaka mzima ujao wa 2023.

(AFP, DPA, Reuters)