1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yapokea mfumo wa ulinzi wa makombora wa Ujerumani

12 Oktoba 2022

Ukraine imepokea mfumo huo wa ulinzi wa angani aina ya T-SLM mnamo wakati Urusi imekuwa ikifanya misururu ya mashambulizi ya makombora katika miji yake.

https://p.dw.com/p/4I4tZ
Flugabwehrsystem IRIS-T SLM
Picha: Shan Yuqi/Xinhua/IMAGO

Ukraine imeipongeza Ujerumani kwa kuipa mfumo wa ulinzi wa makombora.

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Resnikov aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba mwamko mpya wa ulinzi wa angani umeanza. Mfumo wa ulinzi wa angani wa Ujerumani aina ya Iris-Ts uko hapa, Mfumo wa ulinzi wa Marekani aina ya NASAMS unakuja".

Resnikov alimpongeza waziri wa ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht kwa uungwaji mkono wa nchi yake ambayo imekuwa ikijilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi kuanzia Februari.

Ujerumani pia imepanga kuipa Ukraine mifumo minne ya ulinzi wa ardhini dhidi ya makombora yenye thamani ya dola milioni 140.

Mifumo hiyo aina ya Iris-T, inafyatua makombora kutibua ,zana za adui na pia kudungua helikopta na ndege za adui zinazofanya mashambulizi.

Marekani pia imeahidi kuipa Ukraine mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora aina ya NASAMS
Marekani pia imeahidi kuipa Ukraine mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora aina ya NASAMSPicha: Robin Van Lonkhuijsen/ANP/dpa/picture alliance

Moja ya mifumo hiyo aina ya Iris-T SLM inaweza kulinda jiji lenye ukubwa wa kati, kwani makombora yake yanaweza kufyatuliwa urefu wa kilomita 20 na umbali wa hadi kilomita 40.

Tayari wanajeshi wa Ukraine wamepewa mafunzo ya namna ya kutumia zana hizo kutoka Ujerumani.

Urusi yawakamata washukiwa wa mlipuko wa daraja la Crimea

Katika tukio jingine kuhusiana na mzozo huo, Urusi imewakamata washukiwa wanane kwa kuwahusisha na mlipuko kwenye daraja linaloiunganisha na rasi ya Crimea ambayo Urusi ilichukua kwa nguvu miaka kadhaa iliyopita.

Shirika la usalama la Urusi FSB, limesema hayo leo kupitia taarifa na kunukuliwa na mashirika mbalimbali ya Habari.

Taarifa hiyo imesema washukiwa hao ni pamoja na raia watano wa Urusi na wengine watatu ni raia wa Ukraine na Armenia, lakini haikutoa maelezo zaidi kuwahusu.

Kwa nini Daraja la Kerch ni muhimu kwa Urusi na Ukraine?

Taarifa hiyo imeongeza kuwa mabomu yaliyosababisha mlipuko huo yalikuwa na uzito wa kilo 22, 770, na kwamba mabomu hayo yaliingizwa Urusi Oktoba 4, yakiwa yamefichwa kwenye lori, siku mbili kabla ya mlipuko.

Urusi imekuwa ikivurumisha makombora katika miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo mji mkuu Kiev.
Urusi imekuwa ikivurumisha makombora katika miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo mji mkuu Kiev.Picha: State Emergency Service of Ukraine/Handout/REUTERS

Urusi ilisema tukio hilo ililoliita la kigaidi na ambalo lilitokea Jumamosi na kusababisha sehemu ya daraja kuporomoka, lilipangwa na majasusi wa Ukraine.

Kufuatia mlipuko huo, katika siku mbili zilizopita, Urusi imekuwa ikivurumisha makombora katika miji kadhaa ya Ukraine ikiwemo mji mkuu Kiev. Zaidi ya watu 19 wamethibitishwa kuuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa.

Mashambulizi ya Urusi yalaaniwa

Viongozi mbalimbali ulimwenguni wamelaani mifululizo ya mashambuliziya Urusi dhidi ya Ukraine. Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ni miongoni mwa waliolaani mashambulizi hayo na kuwahimiza wanaohusika na vita hivyo kuvimaliza.

"Daima Mungu husikiliza kilio cha maskini wanaomwomba. Roho yake ibadilishe mioyo ya wale walio na hatima ya vita mikononi mwao, ili tufani ya mashambulizi ikome na watu waishi pamoja kwa amani na haki iweze kujengwa upya,” amesema Papa Francis.

(Vyanzo: AFPE, DPAE)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Iddi Ssessanga