1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Khartoum yatikiswa tena na miripuko

4 Julai 2023

Milio ya miripuko imeutikisa kwa mara nyingine mji mkuu wa Sudan, Khartoum, siku chache baada ya jeshi la nchi hiyo kuwahimiza raia kuchukua silaha kupambana na mashambulizi mapya yanayofanywa na RSF.

https://p.dw.com/p/4TP8b
FILE PHOTO: A Sudanese national flag is attached to a machine gun of Paramilitary Rapid Support Forces (RSF) soldiers as they wait for the arrival of Lieutenant General Mohamed Hamdan Dagalo before a meeting
Picha: Umit Bektas/REUTERS

Kulingana na mashuhuda milio ya makombora ilisikika upande wa kaskazini magharibi mwa Khartoum na kusambaa kuelekea katikati na mashariki mwa mji huo.

Mapambano hayo yanajiri baada ya makabiliano mengine siku ya Jumapili kati ya vikosi vinavyoongozwa na mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya wale wa RSF chini ya jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.

Soma pia: Makabiliano yapamba moto Sudan bila kuwepo dalili za maridhiano

Jeshi la nchi hiyo lilitangaza kuwa lipo tayari "kuwapokea na kuwaandaa" wapiganaji wa kujitolea baada ya  jenerali Burhan wiki iliyopita kuwatolea mwito vijana kujiunga na jeshi kuilinda nchi yao.

Nje ya mji mkuu, baadhi ya mapigano mabaya zaidi yameshuhudiwa katika eneo kubwa la magharibi la Darfur, ambapo vikosi vya RSF viliihambulia kambi ya kijeshi huko Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

Kwa mujibu wa Mradi wa kukusanya Data katika Eneo la Migogoro na matukio ya Silaha, tangu Aprili 15 , karibu watu 3,000 wameuawa katika ghasia hizo. Lakini madaktari wanaonya kuwa idadi ya vifo huenda ikawa kubwa zaidi, huku takriban theluthi mbili ya vituo vya afya katika maeneo ya mapigano ikisemekana bado "havifanyi kazi ".

Hali ya raia ikoje?

Gadaref I Konflikt im Sudan
Picha: AFP

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji zinasema takriban watu wengine milioni 2.2 wamekimbia makazi yao na wengine 645,000 wakikimbia na kuvuka mipaka.

Mapigano yamekuwa makali zaidi katika eneo la mji mkuu linalojumuisha Khartoum, Khartoum Kaskazini na Omdurman. Hata hivyo, kuna baadhi ya wakaazi wameamua kubakia.

Mohamed Abdo, mmiliki wa duka la dawa ambalo limedumisha operesheni zake licha mzozo na vita nchini humo, na kuleta matumaini kwa wakaazi huku kukiwa na uhaba wa dawa.

"Nchi haina mustakabali tena, na vijana wamepelekwa kwenye uwanja wa vita. Hakuna elimu au huduma ya matibabu, na miundombinu mingi imeharibiwa katika vita. Kiuhalisia, uporaji na wizi wote unaotokea huwadhuru raia tu na hakuna mshindi katika vita hivi." alisema Mohamed Abdo.

Hali imekuwa ya mbaya Darfur, ambapo vitongoji vyote vimeharibiwa kabisa, miji imezingirwa na miili ya watu waliooza ikizagaa mitaani.

Soma pia: Raia wa Sudan wazidi kuyakimbia mapigano

Hakuna msaada wowote wa kibinadamu umewafikia raia waliokata tamaa, huku makundi ya misaada yakiripoti timu zao zimesimama karibu na nchi jirani ya Chad, wakisubiri njia za kufikisha msaada wa kibinadamu zifunguliwe.

Shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni 13 wako katika "mahitaji makubwa" ya usaidizi wa kibinadamu.

 

//AFP