1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM: Kesi za watuhumiwa wa mauaji ya kivita kuanza The Hague.

6 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFQ2

Umoja wa mataifa umekabidhi majina ya watu 51 kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ili kufanyiwa mashtaka watu wanaotuhumiwa kuhusika na visa vya mauaji ya kinyama, ubakaji na mateso yaliyofanyika katika jimbo la Dafur nchini Sudan.

Hii ni hatua ya kwanza ya kufunguliwa mashtaka kwa wahalifu wa mauaji ya kivita.

Orodha hii inafuatia uchunguzi uliofanywa na tume ya umoja wa mataifa huko Darfur mwaka uliopita kufuatia kukithiri kwa malalamiko ya mauaji, ubakaji na kuchomwa kwa makaazi ya watu.

Kesi hii ya mauaji ya Darfur ndio ya kwanza kuwasilishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

Mapema jana mahakama ya kimataifa ya uhalifu huko The hague ilipokea maboksi yenye stakabadhi za kesi hiyo kutoka Darfur.

Umoja wa mataifa umesema kuwa takriban watu laki moja na elfu themanini wameuwawa na zaidi ya watu millioni mbili wamelazimika kuyahama makaazi yao na kutafuta hifadhi sehemu nyinginezo tangu kuzuka vita vya miaka miwili katika jimbo la Darfur.