1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta azuru mji wa Goma katikati mwa mzozo wa waasi

16 Novemba 2022

Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwasili mjini Goma Jumanne, mnamo wakati mapigano mapya na waasi wa M23 yakizuka eneo la Kibumba, umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa Goma na kusababisha maelfu ya raia kukimbia.

https://p.dw.com/p/4JaoL
DR Kongo Kenias ehem. Präsident Uhuru Kenyatta in Goma
Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, akiwasili kambi ya wakimbizi mjini Goma, katika juhudi zake za upatanishi kusitisha vita vilivyouwa mamia na kuwageuza maelfu kuwa wakimbizi.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Kundi la M23 hivi karibuni limeteka maeneo makubwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini, na kusababisha makumi ya maelfu ya watu kuyatoroka makaazi yao.

Kibumba inachukuliwa kuwa moja ya vikwazo vya mwisho kwa waasi hao kabla ya kufika Goma, ambao ni mji wa kibiashara wa watu milioni moja ulioko kwenye mpaka na Rwanda.

Jumanne mchana, uvumi ulioenea kwamba M23 walikuwa wanakaribia, ulisababisha wimbi jipya na watu kukimbilia kambi ya Kanyaruchinya, kusini mwa Kibumba. Takribani watu 40,000 wanaishi kambini hapo kwa sasa, kulingana na mkuu wake.

 Afisa wa usalama alieomba kutotajwa jina alisema watu walianza kukimbia baada ya kuona wanajeshi wenyewe wakirudi nyuma kuelekea Goma baada ya makabiliano na waasi wa M23.

Soma pia: Kenyatta ataka mamlaka ya Kongo iheshimiwe

Gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Jenerali Constant Ndima, aliwahimiza watu kusalia watulivu Jumanne jioni. "Nataka kuwahakikishia...vikosi tiifu vinamdhibiti adui katika milima ya Kibumba," aliwambia waandishi habari.

DR Kongo Militärischer Gouverneur von Nord-Kivu Constant Ndima
Gavana wa kijeshi wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Constant Ndima anasema jeshi la serikali limemdhibiti adui kwenye milima ya Kibumba.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Mzozo huo umevuruga uhusiano kati ya DRC na jirani yake mdogo zaidi Rwanda, ambayo Kinshasa inaishtumu kuwaunga mkono waasi.

Kenyatta: Siwezi kupuuza nilichokiona

Uhuru Kenyatta, mpatanishi wa jumuiya ya Afrika Mashariki yenye wanachama saba, EAC, aliwasili Goma siku ya Jumanne na kutembelea kambi ya wakimbizi ya Kanyaruchinya.

Aliwaambia waandishi habari Jumanne jioni kwamba simulizi alilozisikia zilikuwa "zinavunja moyo". "Siwezi kupuuza nilichokiona," Kenyatta alisema. "Laazima niseme kwa pande zote: Hamuwezi kujadili katikati mwa janga la kibinadamu".

Soma pia: Vijana wengi wa mkoa wa Kivu Kaskazini kujiandikisha jeshini

Ziara ya Kenyatta nchini DRC ndiyo ya karibuni zaidi katika juhudi za sasa za kidiplomasia kutatua mzozo katika eneo tete la mashariki mwa nchi hiyo maskini.

Rais huyo wa zamani alitua katika mji mkuu wa DRC Kinshasa siku ya Jumapili kwa ajili ya mazungumzo, akifuata katika nyayo za rais wa Angola Joao Lourenco.

Jumuiya ya Afrika Mashariki imeitisha "mazungumzo ya amani" katika mji mkuu wa Kenya Nairobi Novemba 21. Zaidi ya hayo, kanda hiyo imekubali kutuma kikosi cha amani mashariki mwa DRC.

Wanajeshi wa Kenya waliwasili mjini Goma mwishoni mwa wiki, kama sehemu ya operesheni hiyo.

Siku ya Jumatatu, Kenyatta aliyahimiza makundi yenye silaha kuweka chini silaha zao na kurejea kwenye meza ya mazugumzo. "Hakuna kinachoweza kupatikana kupitia mtutu wa bunduki," aliwaambia waandishi habari.

DR Kongo Flüchtlinge aus Flüchtlingslager Kanyaruchikya
Mamia kwa maelfu ya Wacongo wameyakimbia makaazi yao tangu M23 ilipoanzisha mapambano dhidi ya jeshi la serikali ya Congo mnamo mwezi Juni, 2022.Picha: Benjamin Kassembe/DW

Marekani yairai Rwanda kusaidi kukomesha mzozo

Siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema alizungumzia hali nchini Congo na waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda Vincent Biruta, kandoni mwa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa 20 yaliostawi na yanayoinukia kiuchumi duniani, G20, nchini Indonesia.

Soma pia: EAC yatangaza mazungumzo ya amani kwa Congo Mashariki

"Nilitiliza mkazo wasiwasi mkubwa wa Marekani kuhusu kuendelea kwa vurugu mashariki mwa DRC, na kuitolewa wito Rwanda kuchukuwa hatua kuwezesha kupungua kwa vurugu," alisema katika ujumbe wa twitter.

Biruta, kwa upande wake, alitweet kwamba Rwanda imejifunga kwenye mifumo ya kidiplomasia ya kanda inayokusudiwa kuleta amani mashariki mwa DRC, pamoja na kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo.

Zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanarandaranda kwenye kanda hiyo, mengi yake yakiwa urathi wa vita vya kikanda vilivyopamba moto mwishoni mwa karne iliyopita.

Kuibuka upya kwa M23

M23 -- ambalo ni kundi la Kikongo lenye wapiganaji wengi wa jamii ya Watutsi -- lilianza kupata umashuhuri mwaka 2012, baada ya kuuteka kwa muda mji wa Goma kabla ya kufurushwa.

Lakini kundi hilo lilirejea mwishoni mwa 2021 baada ya miaka kadhaa ya diplomasia, likidai DRC imeshindwa kutimiza ahadi ya kuwajumuisha wapiganaji wake kwenye jeshi la taifa, miongoni mwa malalamiko mengine.

Soma pia: Tshisekedi aiandama Rwanda Umoja wa Mataifa

Liliuteka mji wa kimkakati wa Bunagana kwenye mpaka wa Uganda mnamo mwezi Juni. Katika wiki za karibuni, waasi hao wamepata ushindi kadhaa dhidi ya jeshi la Congo, na kusogea karibu kuelekea Goma.

DRC ilimfukuza balozi wa Rwanda mwishoni mwa mwezi Oktoba katikati mwa mashambulizi mapya ya M23. Licha ya ukanushaji rasmi kutoka Kigali, ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo bado haijachapishwa, imeinyoshea Rwanda kidole kuinga mkono M23.

Rwanda inaituhumu serikali ya Congo kwa kula njama na wapiganaji wa Kihutu waliokimbilia nchini humo baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Chanzo: AFPE