1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yasema haitopeleka askari Haiti hadi UN itoe fedha

9 Novemba 2023

Kenya imesema haitapeleka polisi wake nchini Haiti hadi pale mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa yakaporidhia kutoa fedha za kufadhili shughuli za ujumbe huo wa kulinda amani utakaojumuisha pia nchi nyingine kadhaa.

https://p.dw.com/p/4YcxV
Maafisa wa polisi wa Kenya wakishika doria mbele ya jengo la mahakama ya juu mjini Nairobi
Maafisa wa polisi wa Kenya wakishika doria mbele ya jengo la mahakama ya juu mjini NairobiPicha: John Ochieng/SOPA/ZUMA/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki amesema makadirio ya bajeti jumla ya mwaka mmoja kwa ujumbe huo wa amani kwenda Haiti kwa lengo la kurejesha utulivu inafikia dola za Marekani milioni 600.

Kindiki ametoa takwimu hizo alipokuwa akizungumza na kamati ya bunge la taifa kuhusu mpango wa serikali wa kuwapeleka polisi wa Kenya kuongoza ujumbe wa kulinda amani nchini Haiti ambao uliridhiwa na Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Oktoba.

Kenya imeahidi kuchangia askari 1,000 na Kindiki amesema mataifa mengine ambayo hakuyataja pia yameahidi kutoa polisi wao kujiunga na ujumbe huo. Amesema hilo halitofanyika hadi pale bajeti ya kazi hiyo itakaopatikana.

Hata hivyo tayari mahakama nchini Kenya imetoa amri ya kuizuia serikali kupeleka kikosi chochote cha polisi nchini Haiti hadi pale itakapotoa uamuzi juu ya shauri lililofunguliwa na mwanaharakati mmoja wa upinzani kupinga mchakato huo.