1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Viongozi watoa wito wa kuvumiliana kisiasa

Wakio Mbogho4 Aprili 2022

Viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii nchini Kenya wametoa wito wa kuvumiliana miongoni mwa wanasiasa kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

https://p.dw.com/p/49QRV
Uhuru Kenyatta Präsident Kenia Rede Parlament Nairobi
Picha: Simon Maina/AFP via Getty Images

Wito huu unafuatia kisa cha siku ya ijumaa ambapo ndege ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ilirushiwa mawe na vijana. Watu 17 wamekamatwa na Idara ya upelelezi inawachunguza wabunge wawili wa Eldoret. 

Odinga awa rasmi mpizani wa Ruto

Rais Uhuru Kenyatta ameshutumu tukio la Ijumaa la kushambuliwa kwa mgombea urais wa Azimio la umoja Raila Odinga ambapo ndege yake ilipigwa mawe na kundi la vijana eneo la Uasin Gishu. Rais ameonya dhidi ya siasa za chuki akisema kama Raila angejeruhiwa, huenda amani ingevurugika nchini.

Ruto kugombea urais wa Kenya kwa tiketi ya UDA

Siku hiyo Raila alikuwa amehudhuria mazishi ya mfanyibiashara maarufu Jackson Kibor, katika eneo linaloaminika kuwa ngome ya kisiasa ya mpinzani wake, naibu Rais William Ruto.

Tukio la hivi karibuni la ndege aina ya helikopta iliyombeba Raila Odinga kupigwa mawe eneo la Bonde la Ufa, limekosolewa kuwa ishara ya ukosefu wa uvumilivu kisiasa.
Tukio la hivi karibuni la ndege aina ya helikopta iliyombeba Raila Odinga kupigwa mawe eneo la Bonde la Ufa, limekosolewa kuwa ishara ya ukosefu wa uvumilivu kisiasa.Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Uchunguzi unaendelea na kufuatia amri ya Idara ya upelelezi, Wabunge Caleb Kositany wa Soy na Oscar Sudi wa Kapseret pamoja na Spika wa bunge la Uasin Gishu David Kiplagat walifika jijini Nakuru kutoa taarifa.

Siasa za Kenya zachukua mkondo mpya kuelekea uchaguzi Mkuu

Idara hiyo imewataja viongozi hao kama wahusika wakuu wa upangaji wa ghasia hizo zilizosababisha kupasuka kwa kioo cha ndege ya Raila Odinga. Maafisa wa polisi wamewakamata watu 17 kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumza mjini Nakuru, Mbunge Oscar Sudi amelalamika kwamba serikali inatoa haki kwa kuchagua. Anasema matukio kama haya hayapaswi kutumika kusawazisha tofauti za kisiasa.

Naibu wa rais William Ruto ambaye pia anawania urais ni miongoni mwa wale ambao wameshutumu tukio la ndege iliyombeba Raila odinga kushambuliwa kwa mawe.
Naibu wa rais William Ruto ambaye pia anawania urais ni miongoni mwa wale ambao wameshutumu tukio la ndege iliyombeba Raila odinga kushambuliwa kwa mawe.Picha: Reuters/T. Mukoya

Hata hivyo, naibu rais Wiliam Ruto ameomba msamaha kuhusu tukio hilo akisema kila mtu ana haki ya kuomba kura popote nchini bila kushambuliwa. Amewataka waliotekeleza uhalifu huo wakamatwe na wafunguliwe mashtaka.

Mwandishi: Wakio Mbogho, DW, Nakuru.

Mhariri: Iddi Ssessanga