1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga kuwa mrithi wa Uhuru Kenyatta

12 Machi 2022

Kiongozi wa Orange Democratic Movement, ODM,Raila Odinga amepata ridhaa kuipeperusha bendera ya muungano wa Azimio la Umoja katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

https://p.dw.com/p/48OnX
Elfenbeinküste / Ouattara / Odinga
Picha: AP

Raila Odinga aliidhinishwa kuwania urais katika kongamano kuu la Azimio la Umoja lililofanyika jijini Nairobi mapema hii leo.

Akiuhutubia mkutano huo wa kilele,Rais Uhuru Kenyatta alimshukuru kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka kwa kuunga mkono harakati za Raila Odinga na kusema kuwa,”hii ndio siku ambayo tunaianza safari itakayohitimishwa Agosti na itawaunganisha wakenya na nchi kwa jumla.”Rais Kenyatta alikitaja kitendo cha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwa cha kujihini kwa ajili ya ushindi wa muungano wa Azimio.

Kongamano la Wajumbe 300

Uhuru Kenyatta alilihutubia kongamano lililowaleta wajumbe zaidi ya 300 waliokusanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa KICC jijini Nairobi.Rais Kenyatta alieleza kuwa ,”Mola ambariki Raila, rais wa tano wa Kenya kuiongoza Kenya.Nina imani kuwa Raila atalisogeza mbele taifa na kuhakikisha kuwa Kenya itaheshimika ulimwenguni .”

Kwa mtazamo wa rais Uhuru,Raila Odinga ana uwezo wa kupambana na ufisadi kadhalika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa pindi atakapokuwa rais ambaye hatamuacha yeyote nyuma.”Ninaamini hatawaacha ndugu zake nyuma.Kwa sasa tumepata kiongozi wa kweli na serikali mpya itakapoundwa najua Raila atawasikiliza kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka,wa KANU Gideon Moi,Gavana wa Kitui Charity Ngilu na wengine wengine”.

Vyama 26 kushirikiana na Azimio

Kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka aliutangaza msimamo wake rasmi hii leo na kumuunga mkono Raila Odinga wa Orange Democratic,ODM, kuwania urais ifikapo Agosti 9.

Akiwa kwenye uwanja wa Jacaranda ulioko eneo la Embakasi jijini Nairobi alisema,” Niko tayari kumfanyia kampeni Raila Odinga...Raila Tosha.” Hii ni mara ya tatu Kalonzo Musyoka anamuunga mkono Raila Odinga kuwania urais na ana imani kuwa anaweza kupambana na jinamizi la ufisadi linaloizonga Kenya.

Hotuba ya Raila

USA/Kenia Der Keniansiche Präsident Raila Odinga zu Besuch bei Joe Biden
Raila Odinga alipomtembelea Rais Joe BidenPicha: Jim Watson/AFP/Getty Images

Kwenye hotuba yake baada ya kuipata ridhaa ya kuuwakilisha muungano wa Azimio la Umoja kwenye uchaguzi wa Agosti 9, Raila Odinga aliahidi kuwa watadumisha umoja akiwa madarakani,”Wakenya watafahamiana kama ndugu na marafiki.”Kuhusu ushirikiano wake na kiongozi wa Wiper Democratic Kalonzo Musyoka aliweka bayana kuwa,”Mimi na Kalonzo tulikuwa na tofauti kidogo ila tumezijadili na kufikia mwafaka.Tumeamua kushirikiana.Mimi sio kikaragosi cha Uhuru na wala yeye sio changu.”alisisitiza.

Sintofahamu na madai makali

Kabla ya kufikia mwafaka huo,shughuli ya kumtangaza rasmi Raila Odinga kuwa mwakilishi wa Azimio la Umoja kwenye uchaguzi mkuu ilikumbwa na sintofahamu na kucheleweshwa.Duru zinaeleza kuwa Kalonzo Musyoka wa Wiper Democratic alishikilia kuwa anataka apewe nafasi ya mgombea mwenza ambayo inaaminika kuwa imetengewa mwanasiasa atakayetokea eneo la Mlima Kenya lililo na wapiga kura wengi.

Mapambano na Ruto

Kwa mantiki hii, Raila Odinga atachuana na naibu wa rais William Ruto anayeupigia upatu muungano wa Kenya Kwanza.William Ruto yuko kwenye msafara wa kampeni eneo la Mlima Kenya na tayari amepata ridhaa kuipeperusha bendera ya United Democratic Alliance, UDA kwenye uchaguzi wa Agosti 9.Muungano wa Kenya Kwanza unavileta pamoja vyama vikuu vya UDA,Ford-Kenya cha Moses Wetangula,Amani National Congress cha Musalia Mudavadi na vyengine vidogo.

Muungano wa OKA

Muungano wa One Kenya Alliance, OKA,ukiongozwa na Gideon Moi(KANU),Martha Karua(NARC-Kenya) na Cyrus Jirongo(UDP) walitiliana saini makubaliano ya vyama 6 kushirikiana kisiasa siku ya Ijumaa(11.03.2022).Makubaliano hayo yalimhusisha pia Kalonzo Musyoka wa chama cha WIPER Democratic ambaye kwa sasa ametangaza waziwazi kumuunga mkono Raila Odinga kuwania urais kupitia muungano wa Azimio la Umoja.Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika tarhe 9 mwezi wa Agosti mwaka huu.Tayari tume ya uchaguzi na mipaka IEBC imepata nahodha mpya Marjan Hussein Marjan ambaye amekuwa akikaimu nafasi hiyo tangu mwaka 2018.

DW-Nairobi