1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: LSK yapinga agizo la Rais kupeleka majeshi Baringo

20 Februari 2023

Viongozi wa Baringo, moja ya maeneo panapofanyika operesheni ya kukabiliana na majambazi wanaoiba mifugo, wamekikosoa chama cha mawakili nchini humo, LSK, kwa kupinga agizo la rais kuwapeleka majeshi eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4NjvG
Symbolbild I Polizei in Nairobi
Picha: Donwilson Odhiambo/SOPA/ZUMA/picture alliance

Chama cha mawakili hapa Kenya kimeipa serikali siku tatu kuondoa notisi kwenye gazeti rasmi la serikali iliyoamuru kupelekwa kwa majeshi katika kaunti sita za eneo la Bonde la Ufa kukabiliana na majambazi, la sivyo kitaelekea mahakamani kupinga hatua hiyo.

Kupitia taarifa rasmi, rais wa chama hicho, Eric Theuri, amesema hata wakati serikali inapoweka mikakati ya kurejesha amani na usalama katika maeneo hayo, haiwezi kutumia njia zisizoambatana na katiba, na ameitaka serikali kuliwasilisha agizo hilo kwanza kwenye bunge la kitaifa, kujadiliwa na kuidhinishwa na wabunge.

Soma pia: Kenya kutuma wanajeshi kwa operesheni Turkana, Pokot Baringo

Taarifa hiyo inajiri baada ya kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, kuelezea wasiwasi sawia kwamba, kulingana na sheria hatua ya kuwatumia majeshi katika oparesheni, iwe ndani au nje ya nchi, lazima iidhinishwe na bunge la kitaifa.

Kadhalika, wanashauri umuhimu wa sheria kufuatwa kikamilifu ili kuzuia matukio ya ukiukaji wa haki za kibinadamanu.

Hata hivyo, viongozi kutoka Baringo wamekikosoa chama cha LSK kwa kupinga hatua ya Rais kuwaamuru majeshi kuhusika kwenye oparesheni hiyo. Wanasema ujambazi unaoshuhudiwa eneo hilo ni jambo la dharura.

Mnamo Februari 13 mwezi huu, kupitia gazeti rasmi la polisi, serikali ilitoa amri ya kuwatumia majeshi kwenye operesheni maeneo hayo ya Bonde ya Ufa yanayoshuhudia uvamizi wa majambazi wa kuiba mfugo, ili kuzuia maafa zaidi.

Soma pia: Kenya yakabiliwa na kitisho cha njaa, ripoti

Kamishna wa eneo la Bonde la Ufa, Abdi Hassan, ameeleza kwamba tayari zoezi la kuwapokonya majambazi silaha limeanza, na amri ya kutotoka nje inatekelezwa kwa muda wa siku 30 zijazo.

Uvamizi na mauaji yanayotekelezwa na wezi wa mifugo umeshamiri katika maeneo ya Turkana, Samburu, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo na Laikipia.

Licha ya agizo hilo la serikali, mwishoni mwa wiki, wezi wa mifugo walivamia maeneo ya Samburu na Isiolo ambapo waliiba mifugo na kuuwa watu watatu.