1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karatasi za Kura zaanza kuwasili nchini Kenya

Thelma Mwadzaya7 Julai 2022

Shehena ya kwanza ya makaratasi ya kupigia kura imewasili nchini Kenya zikiwa zimebaki siku 32 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika. Tume ya uchaguzi ya IEBC imeweka bayana kuwa hakuna makaratasi ya ziada yatakayochapishwa ila wataifuata idadi ya wapiga kura.

https://p.dw.com/p/4DnZc

Tume ya uchaguzi ya IEBC imeweka bayana kuwa hakuna makaratasi ya ziada yatakayochapishwa ila wataifuata idadi ya wapiga kura.Wakati huohuo Azimio la Umoja One Kenya limekita eneo la Mlima Kenya na Kenya Kwanza ikiwa maeneo ya kaskazini kunadi sera.

Shehena hiyo ya kwanza ya makaratasi ya kupigia kura imewasili kwenye uwanja wa kimataifa wa JKIA muda mfupi baada ya saa nne asubuhi hii.Jumla ya makaratasi 132,722,748 yatachapishwa ambayo ni sawa na moja kwa kila ya wapiga kura milioni 22,120,458 waliosajiliwa kuwachagua wawaniaji wa nafasi sita.

Nafasi hizo ni Rais, Mbunge, mwakilishi wa wanawake, Mwakilishi wa Wadi, Gavana na Seneta.

Mwenyekiti wa Tume asema karatasi za Rais kuwasili mwisho 

Sudan Wahlen Markierung
Picha: AP

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati ameelezea kuwa makaratasi ya kupigia kura ya rais ndiyo yatakayokuwa ya mwisho kuchapishwa.

Chebukati aliweka bayana kuwa makaratasi hayo yatakuwa na alama za usalama kama vile namba asilia mahsusi kwa kila kituo cha kupigia kura.

Kila kituo kitapokea idadi ya makaratasi yanayoendana na wapiga kura waliosajiliwa kwahiyo hakuna nafasi ya wizi au makaratasi ya ziada kuchapishwa.

Yote hayo yakiendelea, kampeni zimeshika kasi na Azimio la Umoja One Kenya imepiga kambi eneo la Mlima Kenya la Kiambu nao Kenya Kwanza wakiendelea kunadi sera eneo la kaskazini.

Zimesalia siku 32 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika ifikapo Agosti.Makaratasi yote muhimu ya uchaguzi yanachapishwa Ugiriki imethibitisha tume ya uchaguzi IEBC.