1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Olaf Scholz asifu msaada wa Japan kwa Ukraine

Daniel Gakuba
28 Aprili 2022

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesifu mchango wa Japan kuisaidia Ukraine inayokabiliwa na uvamizi wa Urusi. Scholz ameyasema hayo baada ya kuwasili mjini Tokyo, kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Japan.

https://p.dw.com/p/4AZvS
Japan Tokio | Olaf Scholz und Fumio Kishida
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani (kushoto) na waziri mkuu wa Ujerumani Fumio Kishida mjini TokyoPicha: Shuji Kajyama/AFP/Getty Images

Akiwa na mwenyeji wake, waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, Kansela Olaf Scholz amesema suala la mshikamano ni lenye kipaumbele miongoni mwa nchi saba za kidemokrasia zinazoongoza kiviwanda, G7 kwa kifupi, hususan wakati huu wa vita vya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Soma Zaidi: Ujerumani, Japan kuimarisha uhusiano wakati wa ziara ya Scholz

Ameisifu Japan akisema tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, kama mshirika wa G7, Japan imesimama bega kwa bega na Ukraine, Ulaya na Marekani, akiongeza mchango huo unapaswa kutambuliwa kwa hali ya kipekee ikizingatiwa kuwa Japan iko mbali sana na Ukraine kieneo.

Ujerumani ni mwenyekiti wa zamu wa kundi la G7 mwaka huu, na mwezi Juni itaandaa mkutano wa kundi hilo katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani.

Nato-Sondergipfel I Russland Ukraine
Viongozi wa Kundi la G7 wanaendelea kuwa na mshikamano wa kuinga mkono UkrainePicha: Sean Kilpatrick/The Canadian Press/AP/picture alliance

Ishara ya mshikamano imara

Scholz amesema kuwa ziara yake nchini Japan ni ishara kwamba Ujerumani na Umoja wa Ulaya wataendeleza ushirikiano na ukanda ulio kati ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Pasifiki ujulikanao kama Indo-Pasifiki. Ameongeza kuwa yeye na mwenyeji wake wamezungumzia kwa kina mzozo wa Ukraine.

''Kuhusiana na uvamizi dhidi ya Ukraine, ambao ni uhalifu mbaya wa kivita unaokiuka sheria za kimataifa, hatua dhidi ya Urusi ambazo tumezijadili leo ina ujumbe wa wazi ambao tunautoa pamoja na Japan na washirika wengine wa kundi la G7,'' amesema Scholz.

Soma zaidi: Putin asema malengo ya uvamizi dhidi ya Ukraine yatatimizwa

Japan ni moja ya nchi tatu za Asia ambazo zimeiwekea Urusi vikwazo, nyingine zikiwa Korea ya Kusini na Singapore. Hata hivyo, sambamba na sera yake ya amani baada ya vita vikuu vya pili, Japan imeipa Ukraine msaada usio wa kivita, unaojumuisha ndege za kijasusi zisizoongozwa na rubani, pamoja na mavazi maalumu yanayovaliwa katika mazingira ya hatari.

BG | Ukraine | Zerstörte russische Panzer
Vita nchini Ukraine ni mojawapo ya vipaumbele vya ziara ya Kansela Olaf Scholz nchini JapanPicha: Vladyslav Musiienko/REUTERS

Japan kusimama pamoja na magharibi dhidi ya Urusi

Kwa upande wake, waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema Japan itasimama pamoja na washirika kama Ujerumani kupinga hatua zozote za kubadilisha maeneo ya kiushawishi katika ukanda wa Indo-Pasifiki, na katika Bahari ya China Kusini.

Soma zaidi: Marekani, Uingereza na Australia zazindua muungano wa usalama

China na Japan zina mvutano wa kieneo katika bahari hiyo, vikiwemo visiwa ambavyo kila nchi inasema ni vyake. Japan pia ina mzozo na Urusi juu ya visiwa vilivyo kaskazini mwa Japan, ambavyo vilichukuliwa kimabavu mwaka 1945 na iliyokuwa Umoja wa Kisovieti.

Kuhusiana na mzozo wa Ukraine kiongozi huyo wa Japana amesema nchi yake itaacha kuagiza makaa ya mawe kutoka Urusi haraka iwezekanavyo, na kutafuta vyanzo mbadala kwa mahitaji yake ya nishati.

afpe, dpae