1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kandanda la wanawake Olimpiki laanza rasmi Alhamis

25 Julai 2024

Mechi za kandanda kwa wanawake katika michezo ya Olimpiki zinaanza Alhamis huku timu 12 tofauti zikicheza mechi zao katika viwanja tofauti kote nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/4ijt1
Timu ya taifa ya kina dada ya Ujerumani
Timu ya taifa ya kina dada ya UjerumaniPicha: Franck Fife/AFP/Getty Images

Timu ya kina dada ya Ujerumani ipo katika kundi B pamoja na Marekani, Zambia na Australia. Ujerumani inaingia uwanjani Alhamis kucheza na Australia huko Marseille katika mechi ya ufunguzi kisha Marekani wavaane na Zambia.

Ujerumani itamkosa kiungo wao muhimu Lena Oberdorf ambaye anauguza jeraha la goti lake la kulia alilolipata katika mechi ya kuwania kufuzu katika Kombe la Ulaya Ujerumani ilipokuwa inacheza na Austria mapema Julai.

Lena Oberdorf baada ya kujeruhiwa dhidi ya Austria
Lena Oberdorf baada ya kujeruhiwa dhidi ya AustriaPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Australia itamkosa mchezaji wao muhimu pia Sam Kerr ambaye ni mmoja wa nyota waliokuwa wanatarajiwa kuonyesha cheche zao katika mashindano hayo. Kerr anayeichezea klabu ya England ya Chelsea, alipata jeraha baya la ACL mwezi Januari na atakuwa nje kwa muda mrefu.

Timu nyengine inayotazamwa kwa karibu ni Uhispania ambayo baada ya kuibuka mabingwa wa dunia kule Australia, sasa wanalenga kunyakua medali ya dhahabu ya Olimpiki.

Uhispania wana vipaji vikubwa kikosini mwao akiwemo mchezaji bora duniani kwa sasa Aitana Bonmati aliyeshinda tuzo ya Ballon d'Or pamoja na Alexia Putellas ambaye aliwahi kuishinda tuzo hiyo mara mbili. Uhispania wanacheza na Japan mjini Nantes katika kundi gumu linalowajumuisha Brazil na Nigeria pia.

Mkongwe wa Brazil ambaye pia aliwahi kushinda tuzo ya mchezaji bora duniani mara sita, Marta, anasema haya ndiyo yatakayokuwa mashindano yake makuu ya mwisho.

Wenyeji Ufaransa watakuwa wanacheza mechi ya ufunguzi ya kundi A siku ya Alhamis dhidi ya Colombia ambao wana mchezaji nyota Linda Caicedo anayesakata kandanda la klabu huko Real Madrid. Wengine walioko kwenye kundi hilo ni Canada na New Zealand.