1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yazindua kampeni ya elimu ya kisheria kwa umma

16 Februari 2023

Serikali ya Tanzania imeanzisha mkakati mpya wa kitaifa wa utoaji msaada wa kisheria kwa wananchi wenye lengo la kuwajengea uwezo ili watambue haki zao na kujipigania.

https://p.dw.com/p/4Na8R
Kenia Nairobi | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania
Picha: Boniface Muthoni/ZUMA Wire/IMAGO

Waziri wa katiba na sheria nchini humo, Damasi Ndumaro amesema kampeni hiyo inatekelezwa kwa mara ya kwanza nchini humo na inafanyika sehemu zote mbili za muungano yaani Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Huduma hiyo ya msaada wa kisheria ambayo inatolewa bure kwa wananchi inasambazwa kuanzia maeneo ya mjini hadi vijijini ambako ndiko kwenye kiini cha mizozo ya ukosefu wa haki kutokana na wengi wao kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya kisheria.

Kampeni hiyo mejikita katika kuwapa uelewa wananchi kuzitambua sheria na haki zao na kisha kuwafungulia mlango juu ya namna ya kuzitekeleza na kupigania haki hizo.

Soma pia:Tume ya Afrika ya haki za binadamu ziarani Tanzania

Maeneo yanayopewa kipaumbele katika awamu hii ya kwanza ya miaka mitatu ni pamoja na masuala yahusuyo unyanyasaji wa kijinsia, haki ya kumiliki ardhi, utatuzi wa migogoro wa njia mbadala na masuala ya haki za binadamu.

Kuminywa haki ndio mzizi wa kampeni

Waziri wa Katiba na Sheria, Damasi Ndumbaro ambaye amezungumza na DW anasema kilio cha wananchi kubinywa haki zaoni cha muda mrefu, lakini sasa mwanga wa matumaini utaanza kujitokeza kupitia mpango huu mpya.

Masai Tansania
Mahakama ya Afrika Mashariki,Arusha TanzaniaPicha: Veronica Natalis/DW

Waziri huyo mwenye dhamana ya sheria na katiba amesema mpango huo umewalazimu pande mbili kuja pamoja kwa maana ya asasi za kiraia zinazotetea haki na serikali, ili kufikia kundi kubwa zaidi.

"Ni kwa mara ya kwanza serikali inaungana na asasi kufanya zoezi kama hili." Aliiambia DW waziri Ndumbaro.

Ameongeza kwamba tayari wamekwishatoa mafunzo kwa watoa msaada wa kisheria katika ngazi ya kijamii wapatao 4,900 na zaidi ya 1,000 kati ya hao wamekwishapata vyeti vyao.

Soma pia:Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo

Aidha amesisitiza kuwa mradi huo wa kutoa elimu ya sheria kwa wananchi utaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu nchi nzima, unatarajiwa kuleta tija kwenye jamii hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudiwa  uelewa mdogo wa masuala ya sheria kwa wananchi.

Asasi za kiraia zaunga mkono juhudi

Hatua hiyo imeungwa mkono na makundi mengi yanayopigania ustawi wa wananchi ikiwamo washiriki wa maaendeleo ambao wameonyoosha mkono kuikaribisha. 

Wengi wanaamini kwamba kupitia kampeni hiyo ambayo pia itafanywa kwa njia ya mtandao sasa wananchi watapatiwa nyenzo zitakazowawezesha kuzifikia haki zao.

Baadhi ya wamasai Tanzania waandamana kupinga kuondoshwa eneo la hifadhi

Kituo cha sheria na haki za binadamu kupitia mkuruguenzi wake mkuu, Anna Henga amesema hatua hiyo inaleta tumaini jingine katika kuwafikia wananchi kwenye mukhtadha wa haki na sheria.

"Hii itakuwa nyongeza kwenye kazi zetu, na tunaahidi kushirikiana na wozara" Alisema Henga alipozungumza na DW.

Soma pia:Mahakama ya EAC yajiandaa kwa rufaa ya Loliondo

Mizozo ya ardhi ambayo wakati mmoja uhusisha kati ya wananchi na taasisi za kiserikali ni mtihani ambao wengi wanasubiri kuona namna kampeni hii itakavyoshughulikia na kupata ufumbuzi wake wa kudumu.