1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jeshi la Bangladesh laingia mtaani kuwadhibiti waandamanaji

20 Julai 2024

Wanajeshi nchini Bangladesh wameendelea kushika doria katika miji mikubwa nchini humo ili kutuliza maandamano ya wanafunzi yanayozidi kuongezeka.

https://p.dw.com/p/4iXh8
 Dhaka | Maandamano
Jeshi nchini Bangladesh limeingia mtaani kuwadhibiti waandamanajiPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Wanajeshi nchini Bangladesh wameendelea kushika doria katika miji mikubwa nchini humo ili kutuliza maandamano ya wanafunzi yanayozidi kuongezeka. Kwa upande mwingine polisi wa  kutuliza ghasia wamewafyatulia risasi waandamanaji waliokaidi amri ya kutotoka nje iliyotolewa na serikali nchini humo mapema hii leo.

Soma zaidi. Polisi Bangladesh watoa amri mpya ya kutotoka nje

Ghasia za wiki hii zimesababisha vifo vya takriban watu 123 hadi sasa, kulingana na takwimu zilizoripotiwa na Shirika la habari la AFP. Amri ya kutotoka nje ilianza kutekelezwa usiku wa manane,  ofisi ya Waziri Mkuu iliwataka wanajeshi kuingia barabarani kushika doria baada ya polisi kushindwa kuwadhibiti waandamanaji wanaopinga upendeleo katika kutolewa nafasi za ajira serikalini.

Tovuti za serikali na magazeti nchini humo yameshindwa kuchapisha taarifa kutokana na kizuizi cha mtandao kote nchini humo kilichowekwa tangu siku ya Alhamisi ambapo mpaka sasa bado kinatumika, Kizuizi hicho kimetatiza mawasiliano ndani na nje ya Bangladesh.