1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM. Vladamir Putin aitaka Iran kuudhihirishia ulimwengu haina njama ya kutengeneza silaha za kinuklia.

29 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFIN

Rais wa Russia, Vladamir Putin, akiwa katika ziara ya kihistoria mashariki ya kati, ameitaka Iran kufanya zaidi kuuhakikishia ulimwengu kwamba mpango wake wa nuklia sio wa kujaribu kuunda silaha za kinuklia.

Alipokutana na viongozi wa Israel, Putin alijaribu kuwahakikishia kwamba mpango wa Russia kutaka kuiuzia Syria makombora na uhusiano wake wa kinuklia na Iran sio tisho kwa Israel. Putin alikubaliana na waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, kushirikiana zaidi katika kubadilishana habari kuhusu ugaidi na katika uchumi.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Russia, Sergei Lavrov, amesema Russia haitaanda mkutano wa kilele kujadili harakati za kutafuta amani katika mashariki ya kati. Amesema pendekezo lililotolewa na rais Putin halikueleweka. Alisema alichopendekeza Putin ni kufikiria kufanyika mkutano wa wataalamu mjini Moscow kujadili mpango wa amani kati ya Israel na Palestina.

Rais Putin anatarajiwa kukutana na rais wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramalaah hii leo kujadili njia za kuisaidi Palestina kuimarisha jeshi lake la walinda usalama. Russia inataka kuipa Palestina helikopta mbili na magari 50 ya jeshi.