1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Jenerali Abdourahamane Tiane ajitangaza kiongozi mpya Niger

Angela Mdungu28 Julai 2023

Mkuu kikosi cha ulinzi wa rais nchini Niger Jenerali Abdourahamane Tiani, amejitangaza kuwa Rais wa baraza la mpito la nchi hiyo. Tiani ametoa tangazo hilo leo kupitia televisheni ya taifa.

https://p.dw.com/p/4UWDA
Jenerali Abdourahamane Tiani
Jenerali Abdourahamane TianiPicha: ORTN/Télé Sahel/AFP/Getty Images

Jenerali Tiani ameomba kuungwa mkono katika uongozi wake, siku mbili baada ya wanajeshi kumpindua na kumshikilia Rais Mohamed Bazoum.

Uongozi huo mpya uliohusika na  mapinduzi, katika taarifa yake iliyotolewa kwa njia ya televisheni umeyatahadharisha mataifa ya kigeni kutoiingilia kijeshi Niger. Taarifa hiyo imesema uingiliaji wowote kijeshi utakabiliwa na matokeo.

Wakati huo huo, Rais wa Kenya William Ruto amelaani mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Niger akiita hatua hiyo kuwa ni kikwazo kikubwa kwa Afrika.

Amesema kuwa Jamhuri ya watu wa Kenya inaungana na dunia kulaani kwa nguvu zote kitendo kisicho cha kikatiba kinachochafua demokrasia kupitia mapinduzi ya kijeshi na inatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Rais Mohamed Bazoum anayeripotiwa kuwa amekamatwa na wajumbe wa kikosi cha ulinzi wa Rais.

Ufaransa yakataa kuutambua uongozi wa kijeshi wa Niger

Katika hatua nyingine, Ufaransa imesema haiwatambui viongozi waliotokana na mapinduzi ya kijeshi ya Niger na kwamba kiongozi halali pekee ni Rais Mohamed Bazoum.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa imeisisitiza Jumuiya ya Kimataifa kutaka kurejeshwa kwa utaratibu wa  kikatiba na serikali iliyowekwa madarakani na wananchi.

Rais Mohamed Bazoum
Rais Mohamed BazoumPicha: Ludovic Marin/AFP

Kutokana na mapinduzi yaliyotokea Niger, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS inatarajiwa kufanya mkutano Jumapili katika mji mkuu wa Nigeria Abuja. Awali Jumuiya hiyo ilitoa wito wa kuachiliwa kwa Rais Bazoum na kutaka katiba ifuatwe.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya wataka Bazoum aachiliwe huru

Niger, imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama tangu Bazoum alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 2021 wakati makundi yenye itikadi kali yaliyokita mizizi yake nchini Mali yalipofanikiwa kudhidibiti baadhi ya maeneo, kuwauwa watu na kusababisha zaidi ya watu milioni 6 kuyahama makazi yao, kote katika ukanda wa Sahel.