1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bazoum aapa kuilinda demokrasia licha ya kupinduliwa

27 Julai 2023

Rais Mohamed Bazoum wa Niger ameapa kuyalinda mafanikio ya kidemokrasia yaliyopiganiwa kwa bidii baada ya kuzuiliwa na jeshi la nchi hiyo lililotangaza kwamba limemuondowa madarakani.

https://p.dw.com/p/4USNW
ARCHIV Niger Niamey | Präsident Mohamed Bazoum
Picha: Boureima Hama/AFP/AP/dpa/picture allaince

Akizungumza kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Bazoum amesema Waniger wanaopenda demokrasia na uhuru wangependa mafanikio hayo yalindwe ipasavyo.

Waziri wake wa mambo ya nje, Niger Hassoumi Massoudu, kupitia kituo cha televisheni cha Ufaransa, France24, amesema Rais Bazoum yu buheri wa afya na akasisitiza kuwa sio jeshi lote lililohusika katika kile alichokiita madai ya mapinduzi.

Soma zaidi: Uchaguzi Niger: Nani zaidi kati ya Mohamed Bazoum na Mahamane Ousmane

Bazoum alishikiliwa na kuzuiwa kutoka katika mji mkuu, Niamey, hapo jana na walinzi wake ambao masaa machache baadaye walitangaza kusimamishwa kwa shughuli katika taasisi zote nchini humo, kufungwa kwa mipaka na marufuku ya kutotembea nje usiku.

Nchi kadhaa za Afrika, mashirika ya kimataifa na marafiki wa Niger katika nchi za Magharibi wamelaani hatua hiyo ya jeshi.