1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Felix Tshisekedi atangazwa mshindi wa urais DRC

31 Desemba 2023

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi ameshinda awamu ya pili ya kwa zaidi ya asilimia 73 ya kura, hii ikiwa ni kulingana na Tume ya Uchaguzi nchini humo, CENI.

https://p.dw.com/p/4akUr
Felix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Picha hii inamuonyesha Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akitoa hotuba kwenye mkutano wa kilele wa uhusiano kati ya Uturuki na Afrika mjini Istanbul, Disemba 18,2023Picha: Isa Terli /AA/picture alliance

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Disemba 20 yalitangazwa katika mji mkuu, Kinshasa jioni ya Jumapili, huku kukiwa na miito kutoka kwa upinzani na baadhi ya makundi ya kiraia kutaka uchaguzi urudiwe, wakidai ilikumbwa na udanganyifu mkubwa na changamoto zinazoibua shaka juu ya uhalali wa matokeo hayo.

Soma pia: Rais Tshisekedi anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa Desemba 20

Tshisekedi alifuatiwa na mfanyabiashara Moise Katumbi, ambaye alipata uungwaji mkono wa silimia 18 ya kura, na Martin Fayulu, aliyepata asilimia 5 huku mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Nobel Dr. Denis Mukwege, aliyepata umaarufu kwa kutibu wanawake waliodhulumiwa kingono mashariki mwa Kongo, akiambulia asilimia 0.22 ya kura zote.

Karibu watu milioni 18 walijitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi huo wa na matokeo haya yatapelekwa kwenye mahakama ya katiba kwa ajili ya uthibitisho, amesema mkuu wa CENI, Denis Kadima.

Hata hivyo, kabla ya matokeo hayo kutangazwa kundi la wagombea wa urais kutoka upande wa upinzani liliitisha maandamano ya kuyapinga matokeo hayo.

Wagombea hao wakubwa wa upinzani walisema kwenye azimio lao la pamoja kwamba wanaupinga uchaguzi huo na matokeo yake na kutaka ufanyike upya chini ya tume mpya ya uchaguzi na tarehe itakayokubaliwa na pande zote.

Lakini serikali ya Kongo tayari ilikataa miito ya kurudiwa uchaguzi.