1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yafanya mashambulizi huko Rafah

22 Februari 2024

Jeshi la Israel limefanya mashambulizi katika mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo ikiwa ni pamoja kuusambaratisha msikiti wa Al Faruq.

https://p.dw.com/p/4ckvZ
Ukanda wa Gaza | Uharibifu katika msikiti wa Al-Farouq huko Rafah
Raia wa Palestina wakishuhudia uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel huko Rafah. Pichani ni mnara wa msikiti wa Al Farouk ulioharibiwa pia na mashambulizi hayo: 22.02.2024Picha: Mohammed talatene/dpa/picture alliance

Mashambulizi hayo ya anga katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza yanajiri baada ya Israel kutishia siku za hivi karibuni kuwa itatuma wanajeshi wake wa ardhini kukabiliana na wanamgambo wa Hamas katika mji huo ambao umekuwa kimbilio la Wapalestina wapatao karibu milioni 1.4 waliokimbia mapigano katika maeneo mingine ya Ukanda huo. Ahmad Abu Mousa, alihamia Rafah akitokea Khan Younis, na sasa haelewi ni  mahali gani palipo salama Gaza:

"Hapo awali nilihamishwa kutoka Khan Yunis, niliambiwa niende Rafah kwa sababu wilaya ya Shabourah ni salama, na tukaja hapa. Je! huu ndio usalama wenyewe? Ni janga. Eneo la makazi lenye ukubwa wa nusu kilomita ya mraba limeharibiwa kabisa."

Ukanda wa Gaza | Mashambulizi huko Rafah
Mashambulizi ya Israel huko Rafah yamesababisha uharibifu wa majengo na msikiti wa Al Farouq: 22.02.2024Picha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Israel imetishia kufanya shambulizi kamili huko Rafah, licha ya miito ya kimataifa kuitaka kuachana na azma hiyo. Viongozi wa mashirika makuu ya misaada ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na  UNHCR, UNICEF, WFP na WHO, waliandika barua ya kusihi usitishaji mapigano mara moja kwa sababu za kiutu na kuonya kwamba vurugu zaidi huko Rafah zitasababisha maafa makubwa.

Juhudi za kusaka usitishwaji mapigano

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh yuko ziarani mjini Cairo, Misri kwa mazungumzo ya kujaribu kufikia makubaliano ya usitishwaji mapigano ambayo yanasubiriwa mno na raia wa Gaza ambao wamekuwa wakishambuliwa kila uchao na kila sehemu.

Soma pia: Marekani yapendekeza kusitishwa mapigano kwa muda Gaza

Israel imesema hii leo kuwa kumekuwepo majaribio mapya yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano hayo, lakini ikatoa sharti la kuachiliwa kwa mateka wote waliosalia mikononi mwa kundi la Hamas.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh
Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh alipokuwa akihudhuria mkutano wa amani huko Algeria:13.10.2022Picha: Fazil Abd Erahim/AA/picture alliance

Mamlaka za Gaza zinazodhibitiwa na Hamas zinataja kuwa watu zaidi ya 29,000 tayari wameuawa, huku wasiwasi wa kimataifa ukiongezeka juu ya idadi kubwa ya vifo vya raia huko Palestina na hatari ya mzozo huu kutanuka na kusambaa katika  eneo zima la Mashariki ya Kati.

Israel imekuwa ikikabiliana na mashambulizi kutoka kwa makundi kama Hezbollah ya Lebanon na wa Houthi wa Yemen, makundi ambayo yanaungwa mkono na Iran. Leo hii, jeshi la Israel limesema mfumo wake wa ulinzi wa anga umefanikiwa kuzuia shambulio la kombora kutoka Bahari ya Shamu ambalo lilikuwa likiulenga mji wa bandari wa Eilat.

(Vyanzo: ap, dpa)