1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza

4 Desemba 2023

Israel imeendeleza mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza wakati wasiwasi wa kimataifa unazidi kuongezeka juu ya vifo vya raia katika vita vinavyoingia mwezi wake wa pili tangu vianze.

https://p.dw.com/p/4ZkMc
Gazastreifen Ausweitung der Bodenoffensive auf den Süden
Athari za mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo la Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, siku ya Jumatatu (Disemba 4).Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Mashambulizi katika eneo hilo yameongezeka tangu siku ya Ijumaa (Disemba 1) baada ya muda wa wiki moja wa kusimamisha mapigano kumalizika.

Siku ya Jumapili (Disemba 3), jeshi la Israel lilitangaza kutanua operesheni yake ya ardhini kwenye Ukanda mzima wa Gaza.

Israel pia ilifanya mashambulizi ya ndege mwishoni mwa juma na imeripoti mfululizo wa makombora kutoka Gaza, ambayo mengi yalizuiwa.

Soma zaidi: Uhaba wa mafuta watatiza shughuli za kiutu Gaza

Pia imewataka watu zaidi kuhama ndani na karibu na mji wa Khan Younis ulio kusini mwa Gaza ili kuepuka mapigano.

Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas katika eneo la Gaza imesema watu zaidi ya 15,500 - nusu yao wakiwa ni wanawake na watoto - wameshauawa katika eneo hilo tangu Oktoba 7.

Marekani, Ujerumani, Israel na nchi nyingine kadhaa zimeiorodhesha Hamas katika orodha ya makundi ya kigaidi.