1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yadai kuwauwa viongozi sita wa Hamas

16 Oktoba 2023

Jeshi la Israel linadai kuwa hadi sasa limeshawauwa viongozi sita wa juu wa kundi la Hamas tangu kuanza vita dhidi ya Ukanda wa Gaza kufuatia uvamizi wa kundi hilo liliouwa na kuwateka nyara wanajeshi na raia kadhaa.

https://p.dw.com/p/4XZp8
Gazastreifen I  Israelischer Luftangriff
Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa leo na Jeshi la Israel (IDF) lililosema viongozi hao wenye vyeo vya juu waliouliwa ni pamoja na maafisa wa kisiasa na kijeshi.

Taarifa ya IDF imewataja pia viongozi wawili wa Hamas ambao waliuawa wiki iliyopita, akiwemo Waziri wa Uchumi wa Hamas, Jawad Abu Shamala, na Zakaria Abu Maamar, ambaye inasemekana alihusika na masuala ya mahusiano ya kimataifa.

Soma zaidi: Wapalestina 2,220 wameuawa katika mashambulizi ya Israel ukanda wa Gaza
UN: Takriban watu milioni moja watoroka makazi yao Gaza

Siku ya Jumapili, Israel iliendeleza usiku kucha mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa lengo la kulisambaratisha kundi la Hamas, lakini viongozi wengi wa kundi hilo linalozingatiwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kama la kigaidi, wanaishi nje ya nchi. 

Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiongezeka kufanikisha hatua ya kupata njia salama katika kivuko cha Rafah, ili kupitisha misaada kuingia Ukanda wa Gaza, baada ya Israel kuamuru kuzingirwa kwa ukanda huo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekanusha taarifa za usitishwaji mapigano na Hamas.