1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel kuwaachia wafungwa 42 na Hamas mateka 14

25 Novemba 2023

Katika makubaliano hayo na kwa muda wa siku nne, Hamas itawaachia mateka 50 huku Israel ikiwaachia wafungwa wapatao 150.

https://p.dw.com/p/4ZRYY
Mateka walioachiwa huru Gaza wawasili Israel
Mateka walioachiwa huru Gaza wawasili IsraelPicha: Ibraheem Abu/REUTERS

Jeshi la magereza la Israel limetoa orodha ya wapalestina 42 wanaotarajiwa kuachiliwa leo huku kundi la Hamas likifahamisha kuwa litawaachia mateka wapatao 14. Katika makubaliano hayo na kwa muda wa siku nne, Hamas itawaachia mateka 50 huku Israel ikiwaachia wafungwa wapatao 150.

Wakati mpango wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas ukiendelea huko Gaza, mapigano yameripotiwa jana usiku kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hezbollah katika mpaka wa Israel na Lebanon, huku meli ya mizigo ya Israel ikishambuliwa katika Bahari ya Hindi.

Katika shambulio la Oktoba 7, Israel inasema Hamas iliwaua watu 1,200 na kuwachukua mateka wengine zaidi ya 200 huku mamlaka za Hamas zikifahamisha kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel tayari yamesababisha vifo vya Wapalestina wapatao 15,000.