1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD : Wanne wahukumiwa kifo kwa njama ya kumuuwa Rais Musharraf

5 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEUt

Mahkama ya kijeshi nchini Pakistan imewahukumu kifo watu wanne kwa kuhusika katika njama ya kumuuwa Rais Pervez Musharraf hapo mwaka 2003.

Wengine wawili wamehukumiwa vifungo vya maisha. Watu hao sita ambao ni wanajeshi wa kikosi cha anga cha Pakistan walijaribu kumuuwa Musharraf kwa kuripuwa daraja karibu na Rawalpindi wakati Rais akipita na msafara wake hapo tarehe 13 Desemba mwaka 2003.Wiki moja baadae kulikuwa na jaribio la pili dhidi ya maisha ya Musharraf wakati washambuliaji wa kujitolea muhanga maisha walipolibamiza gari moja kwenye msafara wake.

Musharraf alinusurika lakini watu 15 walipoteza maisha yao katika jaribio hilo.Wanamgambo watano wa Kiislam walihukumiwa kifo kwa jaribio hilo la pili.

Inadaiwa kwamba mashambulizi yote mawili yalidhaminiwa na kundi la Al Qaeda.