1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yawafukuza wanadiplomasia wa Ujerumani

1 Machi 2023

Serikali ya Iran imewafukuza wanadiplomasia wawili katika ubalozi wa Ujerumani mjini Tehran kujibu hatua ya Ujerumani ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Iran kutoka Ujerumani.

https://p.dw.com/p/4O7Tn
Sprecher des iranischen Außenministeriums Naser Kanaani
Picha: jamaran

Berlin ilichukua hatua hiyo wiki iliyopita baada ya Iran kumhukumu kifo raia wa Iran na Ujerumani na ambaye pia ni mkaazi wa Marekani.

Vyombo vya habari vya Iran vimenukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje Nasser Kanaani akisema wanadiplomasia hao wawili wa Ujerumani wamefukuzwa kutokana na alichokiita, uingiliaji usiokubalika wa Ujerumani katika mambo ya ndani ya Iran na masuala yake ya kimahakama.

SOMA PIA; Ujerumani yakosoa hukumu ya kifo kwa raia wake, Iran

Kanaani ameongeza kusema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasimama kidete dhidi matakwa ya nchi za nje yanayovuka mipaka.

Ujerumani imeikosoa Iran

Iran I Deutsch-Iraner Djamshid Sharmahd in einem Teheraner Revolutionsgericht
Jamshid Sharmahd akiwa kizimbaniPicha: mizan

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani amekosa hatua ya Iran akisema kwamba hatua ya Iran ni ya kiholela na isiyo ya haki.

Ujerumani imeitaka Iran kufutilia mbali hukumu ya kifo iliyotolewa kwa Jamshid Sharmahd ambaye Iran inamtuhumu kwa mashambulizi ya bomu ya mwaka 2008 na kudai kwamba anapanga mashambulizi zaidi.

Anadaiwa pia kushirikiana na maafisa wa kijasusi wa Marekani na Israel na pia kuliongoza kundi la Tondar linaloshutumiwa kutaka kuuangusha utawala wa Iran. Kundi hilo limeorodheshwa kama kundi la kigaidi nchini humo.

Iran | Deutsch-Iraner Djamshid Sharmahd in einem Teheraner Revolutionsgericht
Picha: Koosha Falahi/Mizan/dpa/picture alliance

Mwezi Agosti mwaka 2020 serikali ya Iran ilitangaza kumkamata Sharmahd bila kutoa maelezo zaidi ya ni wapi alipokamatwa, lini hasa na katika mazingira gani. Lakini familia yake inasema alitekwa nyara alipokuwa Dubai na kupelekwa Iran kinyume na matakwa yake.

Baada ya hukumu hiyo mtoto wake wa kike, Gazelle Sharmahd, alisisitiza kuwa babake hana hatia na kutoa wito kwa Mataifa ya Umoja wa Ulaya kuishinikiza Iran kumuachia ili kuokoa maisha ya baba yake ambaye alisema hali yake inaendelea kudhoofika.

SOMA PIA; Umoja wa Ulaya waiwekea Iran vikwazo vipya

Mvutano kati ya Iran na nchi za Magharibi umezidi kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni, na kurudisha nyuma zaidi juhudi ambazo tayari zimekwama za kufufua mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Tehran.

Huku haya yakijiri Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema katika taarifa yake leo Jumatano kwamba inaangalia kwa wasiwasi mkubwa harakati za Iran kujiimarisha kijeshi.

Wizara hiyo pia ilitaja kurutubishwa kwa madini ya Urani huko Fordow na ukandamizaji wa kikatili wa idadi kubwa ya watu wa Iran kama sababu zingine za wasiwasi na kusema Ujerumani ilikuwa katika mazungumzo ya karibu na washirika wa ndani katika eneo hilo, pamoja na Ulaya na Marekani.

 

//Reuters,dpa