1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Iran

Iran kufanya uchaguzi mkuu wa rais mnamo Juni 28

Sylvia Mwehozi
21 Mei 2024

Iran imetangaza kuwa itafanya uchaguzi wa rais mnamo Juni 28, kufuatia kifo cha rais Ebrahim Rais na maafisa wengine katika ajali ya helikopta wakati mazishi yakitarajiwa kufanyika Jumanne.

https://p.dw.com/p/4g59S
Aliyekuwa rais wa Iran Ebrahim Raisi aliyefariki dunia siku ya Jumapili
Aliyekuwa rais wa Iran Ebrahim Raisi aliyefariki dunia siku ya Jumapili katika ajali ya helikoptaPicha: ran's Presidency/WANA via REUTERS

Ripoti za vyombo vya habari vya taifa nchini Iran, zinasema kuwa tarehe hiyo ya uchaguzi, imeidhinishwa wakati wa mkutano wa wakuu wa mihimili mikuu ya serikali. "Kulingana na makubaliano ya awali ya baraza la ulinzi, iliamuliwa kuwa uchaguzi wa 14 wa urais utafanyika Juni 28," imesema taarifa hiyo.

Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, ametangaza siku tano za maombolezo na kumtaja makamu wa rais Mohammad Mokhber, kuwa anachukua majukumu ya rais wa mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.

Maelfu ya waombolezaji wameendelea kumiminika katikati mwa viwanja vya Valiasr Square mjini Tehran kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Raisi na waziri wake wa mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian.Viogozi wa dunia watoa salamu zao za rambirambi kwa Iran baada ya kufiwa na Rais wake

Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber
Rais wa mpito wa Iran Mohammad MokhberPicha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/IMAGO

Shughuli za mazishi zitaanza leo katika eneo la Tabriz kwenye jimbo la mashariki mwa Azerbaijan kabla ya mwili wa Raisi kupelekwa Tehran. Khamenei anatarajiwa kuongoza swala ya kumuaga Raisi Jumanne jioni kabla ya msafara wa mazishi katika mji mkuu.

Iran iliomba usaidizi kwa Marekani wa kuitafuta helkopita

Baada ya helikopta ya Rais wa Iran Ebrahim Raisi kuanguka katika milima karibu na mpaka wa Azerbaijan, Iran iliomba msaada kutoka kwa Washington, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.     

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Matthew Miller amesema waliieleza Iran kwamba Marekani itafanya inavyoweza, lakini ikabainika kuwa hakuna kitu wanachoweza kufanya kutoa usaidizi. Haijabainika ni wapi ombi la Iran la kusaidiwa lilitolewa. Marekani na Iran hazina uhusiano rasmi wa kidiplomasia.Rais wa Iran amefariki katika ajali ya helikopta

Tehran-waombolezaji
Raia wa Iran wakiomboleza kifo cha RaisiPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo, msemaji wa usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani White House John Kirby aliwaambia waandishi wa habari kwamba Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikuwa na "damu mikononi mwake," na kwamba Marekani itaendelea kuiwajibisha Iran kwa kile alichokiita shughuli za kuyumbisha utulivu katika eneo hilo.

Raisi alihusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za nchini Iran na alikuwa ameunga mkono washirika wa kikanda ikiwa ni pamoja na Hamas, aliongeza Kirby.Nchi za Ghuba zaomboleza kifo cha rais wa Iran Ebrahim Raisi

wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikaa kimya kwa dakika moja kumkumbuka Rais Ebrahim Raisi na maafisa wengine kabla ya vikao vya Jumatatu.