1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IPS yamtunuku Annan Tuzo ya Mafanikio kwa mwaka 2006

Mohamed Dahman25 Desemba 2006

Wakati Kofi Annan anaondoka Umoja wa Mataifa wiki hii baada ya kuuongoza umoja huo kwa kipindi cha miaka 10 iliojaa harakati na matukio makuu akiwa kama Katibu Mkuu kutakuwa na tuzo moja ambayo anasema kwa kweli ataibeba mkononi hiyo ni Tuzo ya Mafanikio ya Kimataifa kwa mwaka 2006 ya Shirika la Habari la Inter Press Service (IPS).

https://p.dw.com/p/CHlp
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anayemalizia muda wake wiki hii.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan anayemalizia muda wake wiki hii.Picha: AP

Annan amewaambia takriban wafanyakazi 300 wa Umoja wa Mataifa,mabalozi na wawakilishi wa mashirika yasio ya kiserikali NGOs katika sherehe ya kutunukiwa tuzo ya shirika la habari la IPS iliofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni kwamba baada ya miaka 10 ya msisimko akiwa kama katibu mkuu ni unyenyekevu kuweza kutambuliwa kwa kufanya kile anachopenda kukifanya.

Kabla ya kupokea tuzo hiyo ya IPS Annan amesema kwamba kwa kuwa sasa mabegi yao yote yamefungwa itakuwa ni tuzo moja tu ambayo itabidi aibebe mkononi na hiyo sio Tuzo ya Amani ya Nobel bali ni Tuzo ya Mafanikio ya Kimataifa ya IPS wakati yeye na mke wake Nane wakielekea kwenye mapumziko.

Amesema ameheshimika kweli kwa kupewa tuzo hiyo hususan kwa kuwa inatoka kwa wanahabari duniani ambao walimfanya awe macho saa zote na mara nyengine kumpatia machungu.

Umoja wa Mataifa na Annan kwa pamoja walishinda Tuzo ya Amani ya Nobel hapo mwaka 2001 ambayo ni sifa kuu kabisa kuipokea wakati wa uongozi wake wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Annan amekuwa akipanda cheo kutoka wafanyakazi wa ngazi ya kati katika mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka 44 kwa kuanzia na msaidizi wa katibu mkuu hadi kukwaa ukatibu mkuu wenyewe.

Annan ameliambia shirika la IPS kwamba limekuwa likiripoti juu ya Umoja wa Mataifa kwa mtizamo wa aina yake wa nchi zinazoendelea na kwamba wameupa nafasi uongozi wa Umoja wa Mataifa kusikiliza na wao kuweza kusikika na watu wengi ambao Umoja wa Mataifa unawajali zaidi.

Mkuregenzi Mtendaji wa IPS Mario Lubetkin amesema bodi ya wakuregenzi ya shirika hilo la habari iliamuwa mwezi wa Juali uliopita kumpa Annan tuzo yake ya mwaka 2006 kutokana na mchango wake wa kudumu kwa amani,usalama,maendeleo, uwezeshaji wa kijinsia na haki za binaadamu.

Amesema historia ya miaka 42 ya shirika la IPS ambalo limeendeleza mapambano ya nchi zinazoendelea pia linatambuwa kujifunga kwa Annan katika kusaidia mataifa maskini kabisa duniani katika vita vyao vya kupunguza umaskini uliokithiri na njaa,kuzuwiya kuenea kwa virusi vva HIV na UKIMWI pamoja na kupambana na kudunishwa kwa mazingira kama ilivyotajwa na Malengo ya Maendeleo ya Milinia ya Umoja ya Mataifa.

IPS imekuwa ikifuatilia mafanikio ya Annan na Umoja wa Mataifa na kurepoti kwa miaka yote hiyo kwa kupitia mtandao mkubwa wa waandishi wake zaidi ya 350 katika nchi 150 na katika lugha 22.

Lubetkin amesema wana imani kwamba huduma za Bw. Annan kuwatumikia binaadamu hazitamalizika Desemba 31 na kwamba anataraji watakuwa na fursa ya kumpatia habari na mawasiliano atakayohitaji katika kuelezea dira yake ya usoni kwa watu wa dunia.

Watunukiwa wa zamani wa tuzo ya IPS ambayo ilianzishwa hapo mkwaka 1985 ni pamoja na Graca Machel Mama Rais wa zamani wa Afrika Kusini,Boutros Boutros Ghali katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Marti Ahtisari Rais wa zamani wa Finland.