1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imani potofu, changamoto katika kuudhibiti ugonjwa wa ebola

23 Mei 2018

Wafanyakazi wa afya wanaopambana na ugonjwa wa ebola DRC wamekumbana na changamoto mpya katika juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo - ambayo ni imani kwamba ugonjwa huo ni laana au umetokana na nguvu za kishetani.

https://p.dw.com/p/2yBE6
Kongo Ebola Sicherheitsmaßnahmen in Mbandaka
Picha: Reuters/K. Katombe

Kulingana na daktari mmoja katika eneo la Mbandaka, mchungaji wa kanisa la kianglikana alifariki Jumatano iliyopita, siku chache baada ya kumuombea mtu aliyeugua ugonjwa wa ebola, aliyekwenda kwake kutafuta msaada. Julie Lobali ambaye ni muuguzi aliyeko mstari wa mbele kupambana na mripuko wa ebola, anasema watu wengi wanaamini ugonjwa wa ebola unasababishwa na imani za kishirikina, kwahiyo wanakataa kabisa kutibiwa na kupendelea kuombewa, au wengine kuelekea kwa madaktari wa tiba asilia.

Kongo Ebola Sicherheitsmaßnahmen in Mbandaka
Watoto mjini Bandaka wakiosha mikono kama njia moja ya kujikinga na ugonjwa wa ebola.Picha: Reuters/K. Katombe

Hata hivyo Julie Lobali anasema dhana iliyoenea katika mji wa Mbandaka ni kwamba ebola ilianzia Bikoro kama laana kwa watu waliyokula nyama ya wizi. Akizungumza na shirika la habari la AFP Blandine Mboyo, mkaazi wa wilaya ya Bongondjo mjini Mbandaka amesema muindaji alikilaani kijiji hicho baada ya moja ya mifugo yake kuibiwa.  Mkaazi mwengine Guy Ingila, anasema kuwa amewasikia maafisa katika radio wakisema ugonjwa huo hauna tiba. Ingila anasema ugonjwa huo hauna tiba kwa sababu unatokamana na uchawi.

Lakini kwa madaktari na maafisa wa afya imani hizi zinasababisha wasiwasi mkubwa, na kutatiza juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo hatari wa ebola. Afisaa wa serikali ya DRC  Bavon N'Sa Mputu, amesema ili kuzuwia kabisa kuenea kwa ugonjwa wa ebola ni lazima wawashawishi watu kwamba ugonjwa huu hautokamani na laana, na kuongeza kwamba hili ni jukumu muhimu linalotakiwa kuendeshwa na makanisa nchini humo.

Wataalamu wa utafiti wa tabia za binaadamu kupelekwa Congo kusaidia kampeni ya chanjo ya ebola.

Hapo jana mjini Geneva ,maafisa wa afya kutoka afrika walisema wanawaandaa wataalamu wa utafiti wa tabia za binaadamu katika jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidia katika kampeni ya chanjo ya ebola. 

Wakati huo huo wizara ya afya ya nchini DRC pamoja na shirika la afya duniani WHO, na washirika wengine wako mbioni kuhakikisha chanjo ya ugonjwa wa ebola inaendelezwa licha ya dhana zilizopo. Daktari wa WHO Alhassane Toure anasema wanaendelea kuiunga mkono serikali kupambana na ugonjwa huo hatari.

Kongo Ebola Behandlungszentrum in Bikoro
Baadhi ya wataalamu wanaopambana na ugonjwa wa ebolaPicha: picture-alliance/AP Photos/UNICEF/Mark Naftalin

"Niko hapa kuwasaidia ndugu zangu wa Congo kuudhibiti ugonjwa wa ebola na kusitisha maambukizi yake haraka iwezekanavyo," alisema daktari Toure.

Wizara ya afya imetangaza maambukizi mapya sita ya ugonjwa wa ebola huku visa vingine viwili vipya vya watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo vikiripotiwa hapo jana wakati hatua za chanjo zikiingia siku yake ya tatu hii leo katika juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo katika mji wa Mbandaka ulio na wakaazi milioni moja.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga