1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi yawanaohitaji msaada wa kiutu Kenya waongezeka

Thelma Mwadzaya13 Mei 2022

Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kiutu nchini Kenya imeongezeka kutoka watu 3.1 milioni, mwezi uliopita hadi kufikia watu 3.5 milioni katika kipindi hiki ambacho taifa hilo linakabiliwa na ukame.

https://p.dw.com/p/4BFey
Eco Africa 13.05.2022
Picha: DW

Kitisho kipya cha utapia mlo sugu na ukame mkali kimezuka eneo la kaskazini mwa Kenya linalokabiliana na njaa.Idadi ya wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula imeongezeka kwa kiasi ya nusu milioni inaeleza tathmini mpya.

Kwa sasa serikali inakumbatia mfumo wa kugawa hela badala ya chakula kwa waathiriwa kwani ghala la chakula cha dharura la taifa liko tupu.

Kulingana na taarifa ya mamlaka inayopambana na ukame nchini Kenya,NDMA,idadi ya wanaohitaji chakula cha msaada kwa dharura imeongezeka kutokea milioni 3.1 mwezi uliopita hadi 3.5 katika kipindi kilichofanyiwa tathmini.

Mvua ya msimu wa vuli ilichelewa na ilionyesha imekuwa chache. Ukame katika kaunti 17 kati ya zote 23 za maeneo yanayopata mvua kidogo unaendelea kuwa mkali.

Kaunti 8 za Marsabit,Mandera,Wajir,Samburu,Isiolo,Baringo,Laikipia na Turkana ziko katika hali mbaya sana na zinahitaji msaada wa dharura.

Soma zaidi:UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

Kauli hizo zinaungwa mkono na mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na mratibu wa misaada ya dharura,OCHA, Martin Griffiths anayefanya ziara ya siku mbili nchini Kenya.

Akiwa Turkana ya Kati saa chache zilizopita aliurai ulimwengu kuwakumbuka wakaazi wa Lomoputh. Alisema

" Ulimwengu umesahau madhira wanayopitia wakaazi wa turkana kutokana na Ukame." Aliongeza kuwa ni wakati ambao wakaazi wa eneo hilo wanahitaji mchango wa dunia ili kupata msaada wa kiutu.

Mawaziri mataifa ya G7 wakutana kujadili hali ya chakula ulimwenguni

Mawaziri wa kilimo na chakula wa kundi la mataifa 7 tajiri ulimwenguni,G7 wanakutana mjini Stuttgart hii leo kujadili athari za mzozo wa Ukraine kwenye mfumo mzima wa chakula cha ulimwengu.

Weißenhäuser Strand | Gipfeltreffen G7-Außenminister
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa 7 tajiri ulimwenguni G7Picha: Chris Emil Janßen/IMAGO

Mzozo huo tayari umezua uhaba wa baadhi ya bidhaa za chakula katika mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya.

Ripoti ya Mamlaka ya kupambana na Ukame nchini Kenya, NDMA, imeweka bayana kuwa miti na nyasi zimekauka kwa kiwango kikubw, ikilinganishwa na muda kama huohuo mwaka uliopita.

Soma zaidi:Wafugaji Turkana wabadili mfumo wa maisha kutokana na ukame

mapema mwaka huu ripoti za mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo, shirika la kilimo na chakula  duniani FAO na shirika la mpango wa chakula ulimwenguni WFP zilionya hali ya ukame kusababisha uhaba wa chakula katika maeneo ya pembe ya Afrika.

Wakaazi wairai serikali kuwakumbuka.

Katika maeneo hay ambayo yanakabiliwa na hali ya ukame mifugo katika maeneo hayo im edhoofu, ikikosa nguvu kutokana na uhaba wa chakula, hii ni sababu nyasi zimekauka.

Lolol Lokori ni mkaazi wa Lomoputh na alisisitiza kuwa uhaba wa maji na chakula umewaathiri na hawajapata msaada, katika kipindi hiki kigumu ambacho wanapitia.

Ukame watishia mifugo na kilimo nchini Kenya

Iyanei Kebe ni mama wa watoto wanane na analalamika kuwa wamesahauliwa na serikali ya kaunyo kadhalika mashirika ya misaada.Rhoda Langai ni mwakilishi wa kijiji huko Lomoputh alisema wamepoteza idadi kubwa ya mifugo.

Soma zaidi:Ukame waleta athari jimboni Marsabit nchini Kenya

"Tulikuwa na mifugo imeisha hii ni sababu ya Ukame" Alisema huku akionekana kupoteza tumaini.

Kila unakotazama Turkana ya kati hali inatisha.Mifugo imekonda na mbavu zinahesabika.Watoto wamedhoofika na nyuso za wazazi wao zimesawijika.Baadhi wanaonekana kupoteza tumaini.Upepo mkali tu ndio unaotifua vumbi.