1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yashikwa na hofu ya kukumbwa na ukame

23 Novemba 2021

Nchini Tanzania wakati huu kunashuhudiwa wasiwasi mkubwa ukiongezeka kwa wengi kutokana na hali ya ukame inayoendelea kujitokeza. Wakulima na wafugaji wana hofu kutokana na mvua kutonyesha. 

https://p.dw.com/p/43MU2
farmer shows her dry maize field, Tanzania
Picha: CC/ CIMMYT

Hali hii siyo ya kawaida kwani katika miaka mingi ya nyuma, hadi kufikia msimu kama huu maeneo mengi ya nchi tayari yamepata mvua.

Lakini sasa mambo yanaonekana kubadilika na kwa maana hiyo  wasiwa wasi umekuwa ukiongezeka na wengi wanahisi kwamba huenda madhila yatokanayo na ukame yakagusa karibu sekta zote hasa wakati huu ambako pia kunapoendelea kushuhudiwa mgao wa maji na kupungua kwa nishati ya umeme.

Kumekuwa na miito mbalimbali inayotolewa kunusuru hali hiyo na kutokana na ukumbwa wa janga hilo, waziri wa nishati, January Makamba, ambaye wizara yake inanyoshewa kidole kutokana na mwendo wa kusuasua wa upatikanaji wa nishati ya umeme, anasema kuna haja ya kuwa na tathmini ya kina kuhusu tatizo hilo.

Tanzania inakabiliwa na upungufu wa MW 345 za nishati ya umeme kutokana kushuka kwa kina cha maji katika vyanzo vyake kulikosababishwa na ukame huo. Nako kwenye mgawo wa maji ingawa kwa wakati huu kunashuhudiwa hali ya afuani kiasi, lakini athari zilizosababishwa na mgao huo bado  ni kubwa.

Kenia Rinderhüter und Rinder in Kajiado
Kijana akichunga ng'ombe TanzaniaPicha: dapd

Wakulima, wafugaji pamoja na wajasiliamali wadogowadogo nao wanajikuta wako njia panda wasijue hili na lile kutokana na kitisho cha ukame, na ingawa hivi karibuni mkurugenzi wa mamlaka ya hali ya hewa, Dkt. Agnes Kijazi alionya kuhusu mabadiliko hayo ya hali ya hewa.

Viongozi wa dini wameanza kuchukua jukumu la kujishughulisha na Imani kwa ajili ya kumuomba mola ili kuliepusha taifa na janga hilo la ukame. Mufti mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zuber bin Ally anawataka waimini kwa Imani zao kuweka dua ili nchi ivuke salama katika kipindi hiki.

Kumekuwa na mitazamo mingi inayojadiliwa kuhusiana na hali hiyo ya ukame, huku wengine wakilaumu mamlaka kwa kutoweka vipaumbele mahsusi vya kulinda mazingira na vyanzo vya maji, ingawa wengine wanasema hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo ya shughuli za kibinadamu.