1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki/Syria: Idadi ya watu waliokufa yapindukia elfu 25

11 Februari 2023

Nchini Uturuki pekee watu wapatao 21,000 wamekufa na wengine zaidi ya 80,000 wamejeruhiwa.Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa taarifa hiyo kwenye jimbo la Diyarbakir lililokumbwa na maafa hayo.

https://p.dw.com/p/4NMwS
Türkei Syrien Erdbeben Rettungsarbeiten
Picha: Burak Kara/Getty Images

Mpaka sasa watu wapatao 102,000 wameshahamishwa na kupelekwa sehemu nyingine baada makaazi yao kukumbwa na maafa. Vikosi vya  waokoaji karibu 166,000 vinaendelea na juhudi za uokozi ikiwa pamoja  na waokoaji kutoka nje. 

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus pamoja na mratibu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths wamewasili kwenye mji wa Allepo nchini Syria ambako  watu zaidi ya milioni 5 wameathiriwa na mitetemeko ya ardhi. Shirika la WHO limepeleka tani 35 za dawa muhimu na msaada mwingine unatarajiwa kupelekwa katika siku mbili zijazo.

Watu kadhaa wameokolewa siku tano baada ya maafa kutokea. Msichana mwenye umri wa miaka 4 alikuwa miongoni mwa waliokolewa kwenye mji wa Gaziantep nchini Uturuki. 

Kituo cha radio cha  Uturuki kimearifu kwamba mtoto huyo aliokolewa baada ya kuwa chini ya kifusi kwa muda wa saa 130. Shirika la Uturuki linaloshughulikia hali za dharura limesema mitetemeko mingine 1881 ilifuatia nchini Uturuki.

Soma:Shughuli za uokoaji zaendelea Uturuki na Syria huku vifo vikikaribia 25,000

Wakati huo huo vikosi vya uokozi vya Ujerumani na Austria vimesimamisha shughuli za kuwatafuta watu kwenye jimbo la Hatay la nchini Uturuki kutokana na sababu za kiusalama. Pana taarifa juu ya  kuzuka mivutano kwenye jimbo hilo na milio ya bunduki ilisikika. Hata hivyo vikosi hivyo vya waokozi kutoka Ujerumani na Austria vitaendelea kuwapo ugani.

Vikosi vya waokoaji vyaendelea na juhudi za kuwaokoa watu.
Vikosi vya waokoaji vyaendelea na juhudi za kuwaokoa watu.Picha: Can Ozer/AP Photo/picture alliance

Rais Tayyip Erdogan amesema idara husika zilipaswa kufanya haraka ili kuwasaida wahanga. Rais huyo ameahidi kuanza kazi haraka kwa ajili  ya ujenzi mpya lakini pia amewaonya wahalifu wanaopora mali za watu wakati huu wa maafa.

Misaada pia imewasili nchini Syria licha ya kuwa ya kiwango cha chini kutokana na athari za vita vya muda mrefu.Shughuli za kupeleka misada hiyo zinatatizika hata baada ya serikali ya nchi hiyo kusema mapema wiki hii kwamba itaruhusu misaada kupelekwa.

Mkuu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesifu juhudi zinazofanywa na Uturuki katika kuwashughulikia watu waliokumbwa na maafa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika muda  wa karne.

Mkuu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa Mataifa Martin Griffiths
Mkuu wa kitengo cha misaada cha Umoja wa Mataifa Martin GriffithsPicha: Lev Radin/Pacific Press/IMAGO

Wakati huo huo mwendesha mashtaka wa serikali nchini Uturuki amesema uchunguzi ufafanywa juu ya majengo yaliyosambaratika ili kubainisha iwapo palikuwapo hitilafu katika ujenzi.

Kwa mujibu wa taarifa, polisi nchini Uturuki wanamshilikia mkandarasi mmoja baada ya  kumkamata wakati alipokuwa anasubiri kupanda ndege mjini Istanbul.

Vyanzo:RTRE/AP