1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUturuki

Idadi ya watu waliokufa Uturuki na Syria yapindukia 5,000

7 Februari 2023

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mitetemeko ya ardhi nchini Uturuki na Syria imepindukia watu 5,000 nchini wakati waokoaji wakiendelea na juhudi za kuwatafuta walionusurika.

https://p.dw.com/p/4NBU9
Türkei Erdbeben Kahramanmaras
Picha: IHA/REUTERS

Mamlaka yaUturuki inayoshughulikia maafa na hali za dharura imesema watu wengine zaidi ya 20,000 wamejeruhiwa. Majengo yapatayo 5700 yamesambaratika. Wakati huo huo mkuu wa idara inayoshughulikia maafa na kukabiliana na hali za hatari Orhan Tatar amesema kuwa hali mbaya ya hewa inatatiza juhudi za kuwaokoa watu.

Hali hizo ni pamoja na kuanguka theluji nyingi, mvua na upepo mkali kwenye maeneo yaliyokumbwa na mitetemeko. Baridi pia ni kali kwenye baadhi ya maeneo. Tetemeko la ardhi lililokuwa na nguvu ya 7.7 katika kipimo cha Richter hapo jana liliikumba sehemu ya kusini mashariki mwa Uturuki inayopakana na Syria.

Tetemeko lingine la kipimo cha 7.5 lilifuatia wakati wa mchana.  Kwa mujibu wa mamlaka ya kukabiliana na maafa mitetemeko mingine 243 ilifuatia. Nchini Syria idadi ya watu waliokufa imeongezeka na kufikia watu 1,602 hadi sasa.