1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yasema Iran imeongeza kurutubisha madini ya Urani

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
17 Agosti 2021

Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia duniani IAEA limesema Iran inaendelea kurutubisha madini ya kuwezesha kuundwa silaha za nyuklia na kwamba hatua hiyo inatatiza uwezekano wa kuanzishwa tena mazungumzo.

https://p.dw.com/p/3z4mI
Österreich Wien | IAEA Direktor Rafael Mariano Grossi
Picha: Florian Schroetter/AP Photo/picture alliance

Katika ripoti ya shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, IAEA mkurugenzi mkuu wake Rafael Mariano Grossi amesema Iran imetengeneza gramu 200 ya madini ya Urani yaliyorutubishwa hadi kufikia asilimia 20. Mkurugenzi huyo aliripoti hapo awali kwamba wakaguzi wa shirika la IAEA walithibitisha kwamba Iran walitengeneza gramu 3.5 za madini ya Urani yaliyokwisharutubishwa kwenye mtambo wa nyuklia wa Isfahan. Kulingana na mkataba wa nyukilia wa mwaka 2015, Iran hairuhusiwi kuzalisha na kurutubisha madini hayo. Lengo la mkataba huo ni kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia kwa kuipatia motisha za kiuchumi laiti itautekeleza.

Mtambo wa mafuta wa Isfahan nchini Iran
Mtambo wa mafuta wa Isfahan nchini IranPicha: Akhbare Rooz

Wakati huo huo Marekani imeelezea wasiwasi wake juu ya hatua ya Iran ya kurutubisha madini ya Urani. Hata hivyo Iran imesisitiza kwamba haina mpango wa kuunda silaha za nyuklia na kwamba mpango wake unalenga shabaha za matumizi ya amani tu.

Lakini nchi za Ulaya zilizotia saini mkataba wa nyuklia na Iran (JCPOA) zimesema nchi hiyo haina hoja zenye mashiko za kuutetea mpango wake huo wa matumizi ya amani. Marekani ilijiondoa kutoka kwenye mkataba huo wakati wa Utawala wa Trump mnamo mwaka 2018. Trump alitaka mkataba huo ujadiliwe tena na tangu wakati huo Iran imekuwa inaendelea kuyakiuka makubaliano ya mwaka 2015.

Shabaha ya Iran ni kuwashinikiza wadau wengine watoe motisha zaidi za kiuchumi. Nchi nyingine zilizotiliana saini na Iran, ikiwa pamoja na Urusi na China zimekuwa zinafanya juhudi kwa lengo la kuudumisha mkataba uliofikiwa.

Rais wa Iran Ibrahim Raisi
Rais wa Iran Ibrahim RaisiPicha: Iranian Presidency/ZUMAPRESS/picture alliance

Sasa msimamo wa Marekani umebadilika baada ya rais Joe Biden kuingilia madarakani na rais huyo amesema Marekani iko tayari kurejea kwenye mkataba lakini Iran itapaswa kuzingatia masharti ya mkataba huo. Kwa upande wake Iran imesema inataka vikwazo vyote dhidi yake viondolewe kwanza.

Baada ya kutolewa ripoti hiyo ya Shirika la IAEA, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Ned Price amesema hatua ya Iran itasababisha kufungwa mwanya wa kufanyika mazungumzo yoyote mapya kati ya pande mbili hizo na pia itasababisha Iran kutengwa zaidi. Amesema Marekani haishinikizi tarehe ya mwisho ya mazungumzo hayo lakini ameitaka Iran Itambue kwamba uvumilivu wa Marekani unapungua kila uchao na kwamba dirisha hilo halitabaki wazi kwa muda wote.

Vyanzo://AP/AFP