1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaitaka Afrika kulinda haki za wasichana na wanawake

16 Juni 2022

Leo ni Siku ya mtoto wa kiafrika katika Umoja wa Afrika. Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kuondoa mazoea yenye madhara yanayoathiri Watoto".

https://p.dw.com/p/4CoYZ
Nigeria l Schulmädchen in Kano
Picha: Luis Tato/AFP via Getty Images

 

Katika kuadhimisha siku hiyo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema serikali za Afrika hazipaswi kuvumilia au kuruhusu kisheria ndoa za utotoni, kunyimwa elimu, au ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu dhidi ya wasichana. Badala yake, serikali za Kiafrika zinapaswa kuchukua hatua kali zaidi za kuwalinda wasichana dhidi ya vitendo vinavyokiuka haki zao.

Chanzo cha matendo yenye madhara kwa wasichana na wanawake mara nyingi hutokana na ubaguzi katika maswala ya kimila, kiuchumi, kidini, na kisheria kuhusu jukumu lao katika jamii. Matendo hayo ni pamoja na ndoa za utotoni, ambazo zinaendelea kushamiri barani Afrika hasa katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Nchi 18 kati ya 20 zilizo na viwango vya juu zaidi vya ndoa za utotoni zinapatikana eneo hilo. Asilimia kubwa ya nchi hizo zina viwango vya juu mno vya mimba za utotoni na asilimia kubwa ya wasichana ambao hawajamaliza shule ya upili.

Ndoa za utotoni, kikwazo kwa maendeleo ya wasichana

Rita Nketiah, mtafiti wa haki za wanawake katika shirika hilo la Human Rights Watch amesema wasichana wengi huacha shule kwa sababu hulazimishwa kuolewa na kupata watoto katika wakati muhimu kwa elimu na mustakabali wao. Ameendelea kuwa ndoa za utotoni huzuia wasichana kufanya maamuzi yao wenyewe ya maisha, huvuruga au kukatisha masomo yao, huwafanya wanyanyaswe na kubaguliwa, na pia huwazuia kushiriki kikamilifu katika maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ndoa na viwango vya mimba za utotoni vimeripotiwa kuongezeka barani Afrika katika maeneo mengi ya Kusini mwa Jangwa la Sahara wakati wa janga la Uviko-19. Makadirio ya shirika la kimataifa la watoto UNICEF na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaonyesha ongezeko linaloendelea kutokana na wasichana kuacha shule, familia kupoteza mapato na matatizo zaidi ya kifedha. Soma zaidi :Janga la Covid-19 limepora haki za wanawake na wasichana

Human Rights Watch imesema, kutochukua hatua juu ya ndoa za utotoni kwa serikali kadhaa za Afrika bado ni moja ya vikwazo vikubwa katika jitihada za kulinda haki za wasichana, ikiwa ni pamoja na haki ya elimu. Serikali nyingi za Afrika zimekubali kukabiliana na kukomesha mila potofu dhidi ya wasichana na wanawake, lakini utekelezaji wake unasuasua.

Binti wa Nigeria akitoa machozi.
Binti wa Nigeria akitoa machozi.Picha: Sodiq Adelakun Adekola/Agence-France Presse

Viwango vya juu vya ndoa za utotoni nchini Nigeria

Human Rights Watch iligundua kwamba serikali ya shirikisho na serikali za majimbo nchini Nigeria hazijatekeleza ipasavyo sheria zinazozuia ndoa kabla ya umri wa miaka 18. Katika jimbo la Kano nchini Nigeria, msichana wa miaka 11 aliacha shule baada ya mama yake kufariki na familia yake ilimuoza ili apate mtu wa kumtunza.

Zaidi ya serikali 30 za Kiafrika zimepitisha hatua kadhaa katika miaka ya hivi karibuni ambazo zinalinda haki ya wasichana kubaki shuleni wakiwa na ujauzito au hata baada ya kujifungua. Licha ya hatua kubwa, maafisa wa shule katika nchi nyingi ambazo zina ulinzi wa kisheria, kama vile Kenya na Malawi, bado wanawapiga marufuku wanafunzi hawa katika shule za umma.

Baadhi ya serikali bado hazijapasisha wazi ulinzi wa kisheria na hatua za ziada za kifedha ili kuhakikisha wasichana hawa, ikiwa ni pamoja na wanafunzi walioolewa na walio na watoto, wanapata usaidizi unaohitajika kusalia shuleni. Tanzania, ambayo iliondoa marufuku ya kibaguzi dhidi ya wanafunzi wajawazito au wenye watoto mnamo Novemba 2021, haijaondoa kanuni zinazoruhusu shule kuwafukuza wanafunzi ambao "wameingia kwenye ndoa."

Umoja wa Afrika kuwajibika

Human Rights Watch imesema Umoja wa Afrika unapaswa kushinikiza wito kwa taasisi za Kiafrika za haki za binadamu na kuzitaka nchi zote wanachama kuharamisha ndoa za utotoni na kuhimiza nchi hizo kupasisha sheria na sera zitakazosaidia wasichana kuendelea au kurejea shuleni baada ya kupata mtoto, ili waweze kufaulu kitaaluma.

Ingawa serikali nyingi za Kiafrika zimepiga hatua muhimu katika kupunguza ukosefu wa usawa wa kijinsia katika kupata elimu ya sekondari, wasichana wengi wanaendelea kukabiliwa na vikwazo vinavyowanyima haki yao ya elimu.

Utafiti wa Human Rights Watch nchini Nigeria, Tanzania, na Malawi, miongoni mwa nchi nyingine, uligundua kuwa ada ya masomo na gharama zisizo za moja kwa moja katika shule za sekondari, vinaendelea kuwa mojawapo ya vikwazo vikubwa, hasa kwa wasichana kutoka familia za kipato cha chini na wale wanaokabiliwa na umaskini.

(HRW)