1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yataka DRC kuzuwia chuki dhidi ya Watutsi

4 Desemba 2023

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuchukuwa hatua dhidi ya matukio yanayosababishwa na chuki baada ya mwanajeshi wa Kitutsi kuuawa.

https://p.dw.com/p/4ZlXl
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema Luteni Patrick Gisore Kabongo aliuawa katika mji wa mashariki wa Goma mnamo Novemba 9 katika tukio linalodhaniwa kuwa lilichochewa na chuki za kikabila.  

Mwanajeshi huyo, aliyekuwa na umri wa miaka 42 na aliyekuwa wa kabila la Tutsi kutoka Kivu Kusini, alishutumiwa na waasi wa M23 kwamba tabia zake zilikuwa tofauti na wao, kulingana na Human Rights Watch.

Soma zaidi: Baraza la Usalama latakiwa kuchukua hatua DRCongo

Kundi la M23 ni kundi la waasi linaloongozwa na Watutsi ambalo limeteka maeneo mengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu lianze mashambulizi mwishoni mwa mwaka 2021.

Mtafiti mkuu wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu, Thomas Fessy, amesema kulaani tu hadharani hakuwezi kuzuia uhalifu huo unaochochewa na chuki katika siku za usoni.