1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Raia magharibi mwa Ethiopia waachwa bila ulinzi

31 Agosti 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema kundi lenye silaha liliwaua mamia ya watu wa jamii ya Amhara magharibi mwa jimbo la Oromia nchini Ethiopia mnamo Juni 2022.

https://p.dw.com/p/4GGJf
Äthiopien | Oromiya Region
Picha: G. Fischer/blickwinkel/picture alliance

Takriban miezi mitatu tangu kisa hicho, serikali ya Ethiopia imeshindwa kuwapa wakaazi wa eneo hilo makazi ya kutosha au kushughulikia ipasavyo matatizo mazito ya afya na ulinzi wa raia hao.

Ripoti ya shirika la Human Rights Watch, limesema mnamo Juni 18, wanamgambo waliwavamia raia kwa kuwapiga risasi, miongoni mwao wanawake na watoto wa Amhara kwa muda wa saa nane mfululizo katika vijiji vya Tole na Sene Kebeles.

Takriban watu 400 waliuawa kwenye shambulizi hilo.

Waasi wa Ethiopia wanasema serikali haiwezi 'kuaminiwa'

Wanamgambo hao ambao hawakutambulishwa waliteketeza moto mamia ya nyumba na biashara, kuiba mifugo na kupora mali nyingine. Tathmini ya picha za satelaiti zinathibitisha kuchomwa moto kwa vijiji vitano na uharibifu wa takriban majengo 480. Licha ya tahadhari zilizotolewa, vikosi vya usalama vya serikali vilivyoko karibu havikuwasili hadi saa kadhaa baada ya shambulizi kumalizika.

Laetitia Bader, mkurugenzi wa haki za binadamu katika shirika la Human Rights Watch Pembe ya Afrika, amesema "wavamizi waliokuwa na silaha waliharibu kijiji baada ya kijiji. Wakaangamiza familia nzima kwa ukatili usiomithilika. Haya yalifanyika huku vikosi vya serikali vilivyoko karibu vikionekana kujitia hamnazo". Ameendelea kusema hicho ni kisa cha hivi karibuni cha mauaji ya kimbari ambacho kinahitaji uchunguzi huru na wa haki kutoka kwa serikali ya Ethiopia ili kuwabaini waliohusika na wenye mahitaji wapewe misaada ya kutosha.

Wavamizi walidaiwa kuchoma moto majengo 480, na kupora mali ikiwemo mifugo.
Wavamizi walidaiwa kuchoma moto majengo 480, na kupora mali ikiwemo mifugo.Picha: DW/T. Bukricha

Wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi lenye silaha linalojiita ‘Jeshi la Ukombozi wa Oromo' (OLA) wamekuwa wakipambana magharibi mwa jimbo la Oromia tangu mwaka 2019. Vita hivyo vimesababisha ukiukwaji mbaya wa haki za binadamu dhidi ya jamii ndogo za Oromia. 

Abiy awatuhumu waasi wa Oromo kufanya mauaji ya kimbari

Maafisa wa serikali ya Ethiopia wanalituhumu kundi la OLA kuhusika na shambulizi hilo la mwezi Juni pamoja na mashambulizi mengine. Nalo kundi la OLA linawashutumu wanamgambo wa serikali kuhusika, hivyo limetaka uchunguzi huru kufanywa.

Shirika la Human Rights Watch liliwahoji kwa njia ya simu watu 25 kati ya mwezi Juni na Agosti, miongoni mwao wakiwa mashahidi 19 pamoja na waathiriwa kutoka vijiji vitano vya Gutin, Chekorsa, Silsaw, Begene na vilevile Kijiji jirani cha Sene Kebele

Human Rights Watch pia ilipata orodha ya majina ya wale walioangamizwa, kando na kufanya tathmini ya picha za satelaiti zilizopigwa kabla na baada ya shambulizi.

Kulingana na ripoti ya shirika hilo, makundi yaliyojihami na silaha yalivamia vijiji vya Tole na Sene Kebeles asubuhi ya Juni 18, wakati wanaume walikuwa wameelekea mashambani kwa shughuli zao za kilimo au kushughulikia masuala mengine ya mbali na kuwaacha kina mama na watoto vijijini.

Maafisa wa serikali ya Ethiopia wanalituhumu kundi la OLA kuhusika na shambulizi hilo la mwezi Juni pamoja na mashambulizi mengine. Nalo kundi la OLA linawashutumu wanamgambo wa serikali kuhusika, hivyo limetaka uchunguzi huru kufanywa.
Maafisa wa serikali ya Ethiopia wanalituhumu kundi la OLA kuhusika na shambulizi hilo la mwezi Juni pamoja na mashambulizi mengine. Nalo kundi la OLA linawashutumu wanamgambo wa serikali kuhusika, hivyo limetaka uchunguzi huru kufanywa.Picha: Messay Teklu/DW

Mkulima mmoja kutoka Kijiji cha Gutin amesema mwanzo alisikia milio ya risasi. Ikafuatwa na moshi kutoka Kijiji cha Silsaw. Alipokimbia kuelekea Kijiji chake aligundua kimezingirwa na watu waliokuwa na bunduki. Akawatorosha Watoto wake na kuwaficha kichakani naye akajificha kwenye mti. "Wanamgambo hao walivalia sare na walikuwa na silaha… niliwasikia wakisema waangamize wote, usiwaache. Waue kabisa.”

Mapigano yaripotiwa nchini Ethiopia licha ya wito wa amani

Mwanamke mmoja kutoka Kijiji cha Chekorsa alitoroka pamoja na watoto wake watatu kwa kuingia katika shamba la mahindi lililokuwa karibu. Lakini wavamizi hao walimfyatulia risasi na kumuua mtoto wake mmoja, na mwengine alipigwa risasi ya mgongoni iliyotokea shingoni lakini hakufa. Mtoto mkubwa alinusurika lakini alihitaji wiki mbili za matibabu hospitalini.

Mkuu wa tume ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet pamoja na mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki wametaka uchunguzi huru kufanywa dhidi ya mashambulizi hayo magharibi mwa jimbo la Oromia.

Ofisi ya kiutu katika Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema takriban watu 4, 800 walilazimika kuyahama makwao katika Kijiji cha Tole na Zaidi ya watu 500,000 wameyahama makwao magharibi mwa Oromia kwa sababu ya machafuko.

(HRW)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Mohammed Khelef