1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Kukamatwa Kabuna ni hatua muhimu

19 Mei 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch limesema kukamatwa kwa Félicien Kabuga, mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, ni hatua muhimu inayoashiria uwezekano wa kumfungulia mashtaka.

https://p.dw.com/p/3cTlI
Felicien Kabuga Fahndungsbild
Picha: Public domain

Kwenye ripoti hiyo ya Human Rights Watch, Kabuga aliyekuwa akiishi katika hali ya kujificha nchini Ufaransa hadi kukamatwa kwake mnamo Mei 16, atashtakiwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 huko nchini Rwanda.

Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika, Mausi Segun amesema kukamatwa kwa Félicien Kabuga ni ushindi mkubwa kwa waathirika wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambao wamesubiri kwa zaidi ya miongo miwili kuona haki ikitendeka.

Kabuga alikwepa kukamatwa tangu mwaka 1997, wakati alipofunguliwa mashtaka kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu Rwanda (ICTR).

Sasa hana jinsi, na anatarajiwa kufikishwa mbele ya mahakama ya Umoja wa Mataifa iIiyoanzishwa kwa ajili ya kusikiliza kesi za uhalifu, IRMCT. Kabuga ambaye ni Mhutu na mfanyabiashara anakabiliwa na mashtaka ya kuwafadhili wanamgambo waliowaua Watutsi wapatao 800,000 na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani katika muda wa siku 100 mnamo mwaka 1994. 

Mhakama ya ICRT ina udhaifu

Tangu mwaka huo wa 1994 amekuwa anaishi bila ya kuchuliwa hatua katika nchi za Ujerumani, Ubelgiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Uswisi. Watuhumiwa wengine wawili wa mauaji ya halaiki ya Rwanda, Augustin Bizimana na Protais Mpiranya bado wanasakwa na vyombo vya sheria vya kimataifa.

Ruanda Gedenkstätte an Völkermord in Nyamata
Fuvu kwenye nkumbusho ya mauaji ya kimbari huko Nyamata, ndani ya kanisa Katoliki ambapo maelfu waliuawa 1994 nchini Rwanda.Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Mshauri mwandamizi wa Human Rights Watch, Alison Des Forges mtaalamu wa masula ya Rwanda amechapisha kumbukumbu za mauaji ya kimbari na uhalifu wa nchini Rwanda uliofanywa na wanamgambo wa RPF.

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema katika ripoti yake kwamba kusuasua kwa mahakama ya mjini Arusha ya ICRT katika kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa na wanamgambo wa RPF mnamo 1994 nchini Rwanda ni udhaifu mkubwa ulionyeshwa na mahakama hiyo.

Mfumo wa sheria wa Rwanda pia ulishughulikia kesi za idadi kubwa ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari, katika mahakama za kawaida na katika mahakama za jamii maarufu kama Gacaca.

Viwango vya matokeo ya kesi hizo vimetofautiana sana kutokana na kuingiliwa kati kesi hizo kisiasa na mashinikizo mbalimbali yaliyosababisha vitendo vilivyokiuka haki katika maamuzi ya kesi hizo. Mahakama hizo za jamii, Gacaca zilifikia mwisho wake mwaka 2012.

Chanzo: Human Rights Report