1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya Ebola yaibua hofu mpya duniani

17 Februari 2021

Marekani imesema ulimwengu unapaswa kuchukua juhudi kubwa kupambana na homa hatari ya Ebola na kuizuia haraka iwezekanavyo. Umoja wa Mataifa umeelekeza dola milioni 15 zipelekwe DRC na Guinea kuikabili homa hiyo hatari

https://p.dw.com/p/3pTDV
Demokratische Republik Kongo | Ebola Ausbruch | Krankenhaus
Picha: Al-hadji Kudra Maliro/AP Photo/picture alliance

(Umoja wa Mataifa umetangaza kutowa dola milioni 15 kutoka kwenye mfuko wa fedha za msaada wa dharura, kuisaidia Guinea pamoja na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kukabiliana na mripuko mpya wa homa hatari ya Ebola. Mripuko huo unazusha wasiwasi duniani kote.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la kutowa fedha za kupambana na Ebola limetolewa na mkuu wa shughuli za kibinadamu wa Umoja huo Mark Lowcock na msemaji wa Umoja huo Stephanie Dujarric akasema kwamba fedha hizo dola milioni 15 zitazisaidia nchi zote zilizotajwa ambazo ni Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kupambana na mripuko huo wa Ebola pamoja na kuzisaidia nchi nyinngine jirani kujiandaa.

Dujarric amesema mripuko wa Ebola nchini Congo unashuhudiwa katika eneo lilelile lililowahi kukumbwa na janga hilo mara kadhaa ambapo zaidi ya watu 2,200 wameshakufa katika mripuko uliowahi kutokea mwezi Agosti mwaka 2018 hadi Juni 2020. Ama kuhusu mripuko huo nchini Guinea msemaji wa shirika la afya duniani WHO Margaret Harris anasema visa kadhaa hadi sasa vimethibitishwa.

"Tunafahamu kuna visa 7 vya walioambukizwa Ebola,vitatu vilivyothibitishwa ni vya Guinea na watu watatu miongoni mwao wamekufa. Tumewatambua watu 115 waliowasiliana na wenye Ebola na wengi wao tayari wameshafuatiliwa na hao ni watu 109. Watu hao wako katika mji wa Nzerekore lakini pia Conakry.''

Symbolbild Guinea Ebola
Picha: picture-alliance/dpa/Cabinet Minister De Croo

Hii ni mara ya kwanza Ebola kuingia Guinea tangu uliposhuhudiwa ule mripuko  uliomalizika mwaka 2016.Nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilitangaza rasmi kuwa na janga la Ebola baada ya alau watu watatu kufariki na wengine wanne kuambukizwa.Kufikia sasa nchi jirani za Guinea,SierreLeone na Liberia zimetowa tahadhari kubwa kwa raia wake kuhusiana na hali ya Guinea.

Jumuiya ya kimataifa pia imeingiwa na wasiwasi kuhusu mripuko huo wa Ebola Jana Marekani ilionya kwamba licha ya dunia kukabiliwa na janga la virusi vya Corona juhudi kubwa zinapaswa kuchukuliwa haraka kuzuia homa ya Ebola. Serikali ya rais Joe Biden  kupitia katibu wa habari Jen Psaki imesema  juhudi kubwa na fedha zitumike kuweka usalama wa kiafya duniani kwa kuizuia Ebola kusambaa.

Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa Jake Sullivan nae akazungumza na mabalozi wa Guinea na Congo pamoja na Sierreleone na Liberia kuhusiana na suala hilo na kuonesha kuwa tayari kuzisaidia nchi hizo.Shirika la WHO linashughulika na juhudi za kufahamu zaidi kuhusu kiini na aina ya virusi vya mripuko huo wa homa kali ya Ebola.Mbali na Guinea Umoja wa Mataifa umesema tayari umeziweka kwenye tahadhari nchi sita jirani ya Guinea  ikiwemo Senegal,Guinea Bissau,Mali,Ivory Coast bila shaka Sieerraleone na Liberia.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW