1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisia za vyama vya siasa Tanzania kuhusu demokrasia ya nchi

8 Mei 2023

Vyama vya siasa nchini Tanzania vimeikaribisha hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kuwepo mjadala juu ya mapendekezo yaliyotolewa na kikosi kazi kuhusu demokrasia ya nchi, ikiwamo suala linalohusu katiba mpya.

https://p.dw.com/p/4R2UF
Tansania Daressalam | State House | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin & Gruppenfoto
Picha: Ericky Boniphace/DW

Vikiwa na mitazamo inayokaribiana sana kuhusu kauli hiyo ya Rais Samia, vyama vinaona kuanza kuchomoza kwa nuru mpya ambayo mwishowe itakamilika kwa kupatiakana kwa katiba mpya jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele tangu mchakato wake wa kwanza ukwame mwaka 2014.

Vinasema, kauli ya Rais Samia inaakisi namna kiongozi huyo anavyotembea katika ahadi zake na kusisistiza kwamba, kuwepo kwa majadiliano ya pamoja juu ya yale yaliyopendekezwa na kikosi kazi, ni hatua ambayo inausogeza karibu na jiko la wananchi mchakato wa maridhiano ya kitaifa.

Mbowe: Chadema itaendelea kuikosoa serikali Tanzania

Lakini jambo linalotiwa maanani zaidi na vyama hivyo, ni kuhusu ndoto yao ya muda mrefu ya kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi, vikiamni kwamba hatua hiyo itakuwa mwarobaini wa kutibu donda ndugu kuhusu kuvurugwa matokeo ya uchaguzi.

Kiongozi wa chama cha upinzani Chadema nchini Tanzania (kushoto) akisalimiana na kiongozi wa chama cha upinzani CUF Profesa Ibrahim Lipumba Januari 3, 2023.
Kiongozi wa chama cha upinzani Chadema nchini Tanzania (kushoto) akisalimiana na kiongozi wa chama cha upinzani CUF Profesa Ibrahim Lipumba Januari 3, 2023.Picha: Ericky Boniphace/DW

Kikiweka msimamo wake, chama cha Wananchi-CUF mbali ya kukaribisha mjadala wa pamoja baina ya baraza la vyama vya siasa na msajili wa vyama hivyo, lakini kinakwenda mbali zaidi kutaka maoni ya wananchi kuheshimiwa kuhusu suala la upatikanaji wa katiba mpya

Mhandisi Mohamed Ngulangwa ambaye ni Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, anasema linapokuja suala la katiba mpya, CUF inapendelea kuona tume huru ya uchaguzi inakuwa moja ya kipaumbele kikuu.

Kampeni ya elimu ya kisheria kwa umma yazinduliwa

Katika msimamo wake chama cha ACT-Wazalendo hakijajiweka kando na msimamo wa vyama vingine, lakini kimesisitiza juu ya kuzingatiwa mambo yaliyoanishwa katika mapendekezo ya kikosi kazi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Katika taarifa yake, katibu mkuu wa chama hicho, Addo Shaibu ameorodhesha mambo kama vile sheria mpya ya uchaguzi na sheria  mpya ya vyama vya siasa kuwa ni baadhi ya mambo yanayopaswa kushughulikiwa ndani ya mwaka huu.

Kuandaliwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba ili kuundwa kwa timu ya wataalamu kama ilivyopendekezwa na kikosi kazi, ni eneo lingine ambalo chama hicho ni sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar kimesisitiza.

Haijafahamika ni lini msajili wa vyama vya siasa ataanza kukutana na baraza la vyama vya siasa, lakini wadadi wa mambo wanaona kwamba huenda suala hilo likajitokeza katika siku za hivi karibuni hasa baada ya kusisitizwa na Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na vyama 19 vya siasa