1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za usalama wa michezo ya Olimpiki zapata bigo mjini Athens, Ugiriki

Josephat Charo22 Julai 2004

Mipango ya usalama kwa ajili ya michezo ya Olimpiki huko mjini Athens Ugiriki imepata pigo baada ya majengo rasmi yatakayotumiwa kwa michezo hiyo kushambuliwa huku yakiwa chini ya ulinzi wa polisi.

https://p.dw.com/p/CEHr
Athens Olympiad
Athens OlympiadPicha: AP

Kufikia leo hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo lakini duru za polisi zinasema huenda watu waliotekeleza kitendo hicho wana uhusiano na wapinzani wa mrengo wa kushoto. Msemaji wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba shambulizi hilo halijazusha wasiwasi wowote kuhusu usalama wa michezo hiyo ya Olimpiki. Alieleza kuwa kitendo hicho ni cha kawaida na kilitarajiwa hasa ikizingatiwa hisia walizo nazo watu wa upinzani.

Mabomu ya petroli yalitupwa kwenye jengo la wizara ya utamaduni ya Ugiriki na afisi za Cultural Olympiad mjini Athens. Majengo haya mawili yaliyo chini ya ulinzi mkali wa polisi yako katika eneo linalokaliwa na wanafunzi la Exarchia. Wizara ya utamaduni ina jukumu la kutayarisha michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwezi ujao. Cultural Olympiad ndilo shirika la kiserikali linaloandaa maonyesho ya utamaduni yatakayofanyika pamoja na michezo hiyo kuanzia tarehe 13 hadi 29 mwezi Agosti.

Mabomu mawili ya petroli yalitupwa kwa jengo la wizara ya utamaduni na kusababisha moto ulioufanya ukuta wake kuwa mweusi tititi. Chupa moja haikusababisha moto wowote lakini ilikivunja kioo cha dirisha. Hakuna hasara yoyote nyingine ambayo imeripotiwa.

Shambulizi hili limefanyika wakati ambapo watu wanajadili sana ripoti kwamba walinzi wa kutoka nchi za kigeni walio na silaha wameruhusiwa kuwalinda wanamichezo wao kutokana na wahuni na magaidi. Ugiriki inatuhumiwa kuziruhusu Marekani, Uingereza na Israel kutuma askari wenye silaha kwenye michezo hiyo. Gazeti la New York Times liliripoti hapo awali kwamba Marekani iliishurutisha Ugiriki kuiruhusu kupeleka kikosi maalumu cha wanajeshi 400 na askari, na askari wengine kutoka Uingereza na Israel ili kulinda usalama katika michezo hiyo.

Wapinzani na vyombo vya habari nchini humo wamepinga vikali ulinzi mkali uliopo kwa sasa katika mji wao wa Athens. Hawafurahishwi na vile Marekani inavyoingilia usalama wa ndani wa nchi yao huku wakidai wanataka kusadia. Ukweli wa mambo ni kwamba Marekani na Uingereza hazina imani na mipango ya usalama kwenye michezo hiyo, jambo ambalo limewaudhi wagiriki wengi hasa wale wanaounga mkono upinzani.

Tangu sheria kali za usalama zilipoanza kutekelezwa katika michezo ya Olimpiki, mashambulizi haya ambayo hufanywa mara kwa mara mjini Athens, yamepungua sana. Mnamo tarehe 5 mwezi Mei mwaka huu, mabomu matatu madogo yalirushwa kwenye kituo cha polisi mjini Athens na kusababisha uharibifu mdogo. Kundi la kigiriki liitwalo Revolutionary Struggle lilidai kutekeleza shambulizi hilo.

Majuma mawili baadaye, tarehe 19 Mei askari waliharibu kifaa mfano wa bomu ambacho kilikuwa kimetegwa chini ya gari ndogo iliyokuwa mbele ya nyumba ya mfanyakazi wa kampuni ya Uingereza iitwayo British Rover. Kundi lingine la Revolutionary Popular Action lilidai kuhusika na harakati hizo ambazo hazikufaulu kutimiza lengo lake.

Polisi nchini Ugiriki imesema kwamba makundi haya mawili hayana uhusiano wowote na ugaidi wa kimataifa hivyo basi harakati zao hazijahatarisha usalama wa michezo hiyo. Serikali ya Ugiriki inatarajia kutumia kadri dola bilioni 1.5 kwa usalama wa michezo ya Olimpiki ambayo ni ya kwanza kufanyika tangu shambulizi la Septemba 11 mwaka wa 2001 dhidi ya Marekani.

Kulingana na matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa, karibu wagiriki robo tatu hawana wasiwasi wowote kuhusu uwezekano wa mashambulizi kufanyika katika michezo hiyo.