1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yalegeza vikwazo vya usafiri kwa nchi tisa

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
4 Januari 2022

Duniani kote nchi zinapambana na ongezeko la watu wanougua COVID-19, hali inayochochewa na kirusi kipya cha Omicron. Wakati huo huo watu kadhaa Ujerumani waandamana kupinga masharti ya kuzuia kuenea maambukizi ya corona.

https://p.dw.com/p/4582w
Einreise EU | Covid-19: Airport Corona Testing
Picha: Zumapress/picture alliance

Ujerumani imelegeza vikwazo vya corona kwa wasafiri wanaoingia nchini humo vilivyowekwa dhidi ya nchi tisa zikiwemo Uingereza na Afrika Kusini kutokana na nchi hizo kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi vya omicron. Taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani ya Robert Koch (RKI) imethibitisha kwamba kuanzia leo Jumanne, nchi zaidi hazitawekwa kwenye orodha ya tahadhari kubwa kwa sababu ya kirusi cha omicron. Ingawa bado kuna tahadhari kubwa zitakazofuatwa kwa wasafiri lakini watu waliochanjwa watakuwa na wepesi mkubwa katika safari zao za kuingia Ujerumani.

Wakati huo huo polisi nchini Ujerumani wameelezea juu ya kutokea vurugu za hapa na pale kwenye maandamano ya kupinga vikwazo vya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi ya corona. Mwandamanaji mmoja katika mji wa mashariki wa Lichtenstein amemng'ata meno afisa wa polisi na mtu mwingine alijaribu kuiba silaha kutoka kwa afisa wa polisi.

Polisi wakikabiliana na waandamanji wanaopinga masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona katika mji wa Magdeburg
Polisi wakikabiliana na waandamanji wanaopinga masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona katika mji wa MagdeburgPicha: Klaus-Dietmar Gabbert/dpa/picture alliance

Huko Magdeburg ambao ni mji mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt, waandamanaji waliwarushia polisi chupa na fataki. Hakuna afisa aliyejeruhiwa, polisi wamesema. Maandamano hayo yalifanyika kabla ya mkutano wa leo Jumanne wa jopo la wataalam wa Ujerumani ambao wanatarajiwa kuwasilisha mapendekezo mapya kwa serikali kuhusu namna ya kukabiliana na mlipuko wa janga la corona. Mkutano wa viongozi wa serikali kuu na wa majimbo umepangwa kufanyika siku ya Ijumaa.

Marekani

Nchini Marekani, shule nyingi zimeamua kuchelewesha wanafunzi kurudi shuleni kutokana na maambukizi ya corona na wakati huo huo Bunge la Marekani lilikumbwa na hali isiyokuwa ya kawaida ambapo maambukizi ya corona yameongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mujibu wa tovuti ya bunge maambukizi yalipanda hadi asilimia 13 kutoka asilimia iliyokuwepo mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana.

Brazil

Kampuni za meli za wasafiri nchini Brazil zitasimamisha kutoa huduma zake hadi Januari 21. Chama kinachosimamia sekta ya hiyo kisema hay baada wizara ya afya kupendekeza kwa kampuni hizo za meli zisimamishe shughuli za usafiri ili kuepuka maambukizi zaidi.

Maambukizi ya siku hadi siku yameongezeka nchini India. Hali hii ilianza kujitokeza tangu mapema mwezi  Septemba mwaka jana na mmoja wa watu walioambukizwa ni waziri kiongozi wa Delhi, Arvind Kejriwal, ambaye alikuwa kwenye mkutano wa uchaguzi wa jana Jumatatu bila ya kuvaa barakoa.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na mkewe Isaura kwenye kampeni za uchaguzi mwaka 2019 mjini Maputo
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na mkewe Isaura kwenye kampeni za uchaguzi mwaka 2019 mjini MaputoPicha: Ferhat Momade/AP Photo/picture alliance

Kwingineko ofisi ya rais wa Msumbiji imesema Rais Filipe Nyusi na mkewe Isaura Nyusi wamethibitishwa kuwa na COVID-19 na kwa sasa wanajitenga.

Na shirika la afya duniani, WHO, limesema ushahidi zaidi unaonesha kwamba kirusi kipya cha Omicron kinaathiri upumuaji katika sehemu ya juu ya mwili wa mwanadamu tofauti na aina zingine za virusi vya corona ambavyo husababisha nimonia kali.  Meneja wa WHO anayesimamia hali ya maambukizi, Abdi Mahamud amesema mjini Geneva, kuwa utafiti huo unaweza kuwa ni habari njema.

Chanzo:RTRE/AP/ https://p.dw.com/p/456K3