1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya haki za binadamu Afrika hairidhishi

Veronica Natalis
25 Oktoba 2023

Mkutano wa 77 wa haki za binadamu unafanyika mjini Arusha Tanzania, ambao unataja mapinduzi ya kijeshi na vita katika baadhi ya mataifa ya Afrika kumesababisha ukiukwaji wa haki za binadamu, kando na mambo mengine.

https://p.dw.com/p/4Y1UU
Wadau wa Haki za binadamu na maendeleo wakiwa katika mkutano mjini Arusha, Tanzania
Wadau wa Haki za binadamu na maendeleo wakiwa katika mkutano ArushaPicha: Veronica Natalis/DW

Mkutano huo unaotarajiwa kukamilika tarehe tisa ya mwezi huu wa Oktoba unaowakutanisha wadau wa haki za binadamu kutoka nchi mbali mbali za Afrika umezitupia lawama baadhi ya serikali za Afrika pamoja na jumuiya za kikanda, kwa kushindwa kuwajibika kuwalinda raia dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu. 

Baadhi ya matukio yaliyobainishwa na mkutano huo ambayo yanaashiria nchi kukwepa uwajibikajiwa kulinda haki za binadamu, ni pamoja na nchi kujitoa katika itifaki ya mahakama ya Afrika ya haki za binadamu,  inayoruhusu raia na mashirika binafsi kuwaruhusu watu wake kufungua kesi zinazohusu haki za binadamu.

Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi nne zilizojitoa katika mkataba huo, imeendelea kushikilia msimamo kuwa inafanya vizuri katika ulinzi wa haki za binadamu.

Soma pia:Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa akemea mapinduzi barani Afrika akisema sio suluhu

Matukio mengine ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyotajwa na mkutano huo ni pamoja na  migogoro ya ardhi na makazi baina ya serikali na wananchi kama vile mgogoro uliopo kati ya serikali ya Tanzania na jamii ya wafugaji ya Maasai, mapinduzi ya kijeshi yaliyozikumba baadhi ya nchi za Afrika hivi karibuni, pamoja na hali ya kiusalama ya eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Dr. Enno: Wananchi wanazuiliwa kufungua kesi

Awali akitoa hotuba kwa niaba ya Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu msajili wa Mahakama hiyo Dr. Robert Enno alibainisha kuwa  serikali za Afrika bado zinasua sua katika ulinzi wa haki za binadamu. 

Mahakama ya Afrika Haki za Binadamu
Mahakama ya Afrika Haki za BinadamuPicha: Veronica Natalis/DW

Alisema kwa sauti moja mataifa ya Afrika yanakubaliana kwamba ulinzi wa haki za binadamu ni jukumu la nchi wanachama, lakini nchi haziwezi kufikia lengo la kulinda haki za binadamu kama hazifuati taratibu zinazotakiwa.

Aidha alihoji juu ya nchi wanachama kuwazuia raia wake na mashirika binafsi kufungua kesi dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu.

Soma pia:Mahakama ya Haki Afrika:Tunisia iruhusu wafungwa kuwasiliana

"Tunawezaje kusema tunalinda haki za binadamu wakati maamuzi ya Mahakam hii hayatekelezwi nan chi wanachama?” Alihoji Dr. Enno.

Japo kimekuwa ni kilio cha muda mrefu, lakini washiriki wa mkutano huo wameendelea kuzikosoa baadhi ya serikali za nchi za Afrika kwa namna zinavyoshughulikia ulinzi wa haki za binadamu.

Kikao hiki cha kila mwaka kimewajumuisha wadau wa haki za binadamu wapatao 1000 kutoka serikali za nchi mbali mbali za Afrika pamoja na  jumuiya ya kikanda na kimataifa.   

Waandamanaji wadai mageuzi na haki Sudan