1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Guterres, wajumbe kujadili mzozo wa Afghanistan

1 Mei 2023

Mazungumzo kuhusu mgogoro wa Afghanistan yanafanyika leo (01.05.2023) Doha, Qatar. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atawakusanya wanadiplomasia wa kimataifa katika eneo la siri mjini Doha.

https://p.dw.com/p/4Qjs1
Somalia Mogadischu Besuch UN-Generalsekretär Guterres
Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Ukichukuliwa kuwa mgogoro mkubwa kabisa wa kibinadamu na Umoja na Mataifa, mtihani unaomkabili Guterres umezidi kufanywa kuwa mgumu na hatua ya watawala wa Taliban kuwapiga marufuku wasichana wasiende shule na wanawake wengi wasifanye kazi, hata na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa wanadiplomasia, serikali ya Taliban iliyotwaa madaraka mnamo Agosti 2021 haitawakilishwa kwenye mazungumzo ya mjini Doha yanayohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 25 na mashirika ya kimataifa.

Kabla mazungumzo yanayoanza leo kundi la wanawake walifanya maandamano katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul Jumamosi iliyopita kupinga kutambuliwa kwa aina yoyote kwa serikali ya Taliban, lakini Umoja wa Mataifa na dola za Magharibi zimeshikilia suala hili halitajadiliwa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Vedant Patel amesema aina yoyote ya kuitambua Taliban haipo katika ajenda ya mazungumzo.

Mbali na kuthibitisha kwamba utawala wa Taliban haupo katika orodha ya washiriki wa mkutano wa Doha, Umoja wa Mataifa umekataa kutoa maelezo ya kina yakiwemo kuhusu eneo kunakofanyika mkutano mjini Doha au nani atakayejumuika na Guterres katika mazungumzo hayo.

Mikutano bila Taliban haitakuwa na tija

Naibu waziri wa Taliban anayeshughulikia masuala ya wakimbiz Mohammad Arsala Kharoti alisema jana Jumapli kwamba mikutano ya aina hiyo haitakuwa na tija yoyote. Akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP katika uwanja wa ndege wa mjini Kabul, Kharoti amesema ili mradi hawatajenga mahusiano na Afghanistan na hakuna uwakilishi, mikutano kama hii haitakuwa na mafanikio kwa kiwango kikubwa.

Wanadiplomasia wanasema akiwa mjini Doha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia anatarajiwa kutoa taarifa mpya ya tathmini ya operesheni ya utoaji misaada nchini Afghanistan. Operesheni hiyo iianza baada ya amri kutolewa mwezi Aprili kufuatia hatua ya mamlaka kuwapiga marufuku wanawake wasifanye kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Afghanistan Kabul | Afghanische Frauen protestieren für ihre Rechte trotz Unterdrückung
Wanawake wa Afghanistan wakiandama Jumamosi 29.04.2023 mjini KabulPicha: AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umesema unakabliwa na mtihani mgumu ikiwa uendelee mbele na operesheni yake katika nchi hiyo ya wakazi milioni 38. Ikikabiliwa na changamoto nyingi kutokana na vita vya Ukraine na migogoro mingi ya kimataifa, dola wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ziliungana pamoja Alhamisi iliyopita kulaani marufuku dhidi ya wanawake na wasichana wa Afghanistan na kuzitaka nchi zote zitafute kwa haraka kufutwa kwa sera hizo.

Wizara ya mambo ya nje ya Afghanistan ilikataa wito huo na ikasema marufuku hiyo ni suala la ndani la kijamii la Afghanistan. Richard Gowan, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa katika shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo amesema umoja huo uko kwenye mtego kuhusu Afghanistan. Amesema Guterres ana kibarua kipevu cha kutafuta ufumbuzi, anatakiwa atafute njia kuhakikisha msaada unaendelea kupelekwa Afghanistan, lakini marufuku dhidi ya wanawake ni pigo kubwa kwa uwezo wa Umoja wa Mataifa kufanya kazi nchini humo. Gowan amesema jumuiya ya kimataifa inataka Umoja wa Mataifa uendelee kubaki Afghanistan, licha ya tofauti nyingi zilizopo miongoni mwa nchi wanachama wa baraza la usalama.

Mapendekezo kuwasilishwa

Umoja wa Mataifa umeashiria juu ya mapendekezo ambayo yumkini yakawasilishwa katika kikao cha Doha. Msemaji wa umoja huo Stephanie Dujarric alisema Ijumaa iliyopita kwamba nia ni kuchagiza ushirikishwaji wa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono malengo ya pamoja kuhakikisha njia thabiti ya kusonga mbele kuhusu suala la Afghanistan inapatikana.

Umoja wa Mataifa pia unataka umoja au ujumbe wa pamoja kuhusu haki za wanawake na haki za binadamu, mapambano dhidi ya ugaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya. Dujarric amesisitiza kutambuliwa Taliban sio suala la kujadili. Ikiwa Taliban watachukua kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ni suala ambalo Baraza kuu la Umoja wa Mataifa linatakiwa liamue. Hata hivyo Umoja wa Mataifa na makundi mengine yamekuwa yakifanya mazungumzo ya jinsi ya kuwashikirikisha watawala wa Taliban na pengne kuwapa vishawishi kwa ajili ya mageuzi. Mapendekezo yamewasilishwa kwamba Marekani itafakari kuilegezea vikwazo Afghanistan.

(afpe)