1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi wafadhili kutoa dola bilioni 12 kuisaidia Afghanistan

Sylvia Mwehozi
25 Novemba 2020

Wajumbe katika kongamano la wafadhili wa kimataifa juu ya Afghanistan, wameahidi kutoa kiasi cha dola bilioni 12, ndani ya miaka minne ijayo ili kuisadia nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

https://p.dw.com/p/3lmgx
Schweiz | Online-Geberkonferenz für Afghanistan
Picha: Valentin Flauraud/dpa/picture alliance

Katika mkutano huo uliofanyika mjini Geneva kwa njia ya vidio, nchi wafadhili zimekubali kuendelea kuisadia nchi hiyo ambayo imegubikwa na machafuko baina ya wapiganaji wa Taliban na serikali, ufisadi mkubwa na kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani.

Waziri wa ushirikiano wa maendeleo na biashara ya kigeni wa Finland Ville Skinarri, alisema nchi wafadhili wameahidi kutoa dola bilioni 3 mwaka ujao, huku kiasi hicho kikitarajiwa kuendelea kutolewa kila mwaka hadi kufikia 2024 na hivyo kufanya jumla ya ufadhili kufikia dola bilioni 12.

Nchi nyingi zimetoa masharti kwa Afghanistan juu ya kuheshimu mchakato wa amani na kutaka uongozi bora ili kuboresha demokrasia na kupambana na ufisadi. Jumuiya ya kimataifa ilitaka pia "usitishwaji wa kudumu wa mapigano", wakati watu wasiopungua 14 wakiuawa katikati mwa Afghanistan pale milipuko miwili ilipotokea katika mji wa kihistoria wa Bamiyan.Afghanistan yatangaza timu ya mazungumzo na Taliban

Waziri wa mambo ya kigeni wa Afghanistan Mohammad Haneef Atmar amesifu kiasi kilichopatikana, akiongeza kuwa " ni muhimu zaidi kwasababu mchango huo umekuja wakati ambapo hakuna taifa lolote ambalo halijaathirika na COVID-19 katika uchumi na mapato yake".

Afghanistan Bamiyan | Anschlag
Afisa wa usalama wa Afghanistan akiwasili eneo la mlipuko BamiyanPicha: AFP/Getty Images

"Ni muhimu kwamba wamegusia ukweli juu ya kiwango cha sasa cha vurugu kisichokubalika kabisa, na kutakuwa na usitishaji mapigano mara moja. Ni ujumbe mzito kwa Taliban kwamba sio tu watu wa Afghanistan ambao wanadai mapigano kusitishwa mara moja, sasa", alisema Atmar.

Hapo Jumanne, rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, aliwahimiza washirika wa kimataifa kudumisha michango yao ya kifedha, akiongeza kuwa ufadhili uliopita umesaidia sana kuongeza elimu kwa wanawake, kuboresha usambazaji wa umeme pamoja na kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza "dhamira ya taifa hilo ya kuleta maendeleo na mageuzi" akisisitiza kwamba taasisi hiyo inasimama na Afghanstan kuelekea njia ya amani, maendeleo na kujitegema.

Mazungumzo katika mji mkuu wa Qatar wa Doha baina ya serikali ya Afghanistan na wapiganaji wa Taliban yalianza mwezi Septemba lakini yamekuwa yakisuasua huku vurugu zikiibuka tena kote nchini. Nchi wafadhili hukutana kila baada ya miaka minne kwa ajili ya kukusanya fedha kuisaidia Afghanistan, ambayo inategemea kwa kiasi kikubwa usaidizi wa kigeni licha ya miaka kadhaa ya kuahidi mageuzi na kukuza uchumi.