1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza: Mamia ya wafanyakazi wa UNRWA wasimamishwa kazi

2 Agosti 2018

Wasiwasi umeongezeka katika Ukanda wa Gaza baada ya shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa wakimbizi wa Palestina kuwasimamisha kazi mamia ya watu baada ya Marekani kulipunguzia fedha shirika hilo.

https://p.dw.com/p/32WjP
Lastwagen Kerem Shalom  Gaza Schließung
Picha: picture-alliance/Photoshot/K. Omar

Ajira zipatazo 250 ziliondolewa mnamo wiki iliyopita jambo lililosababisha maandamano katika Ukanda wa Gaza. Rais wa Marekani Donald Trump aliamua kupunguza ufadhili wa mamilioni ya dola. Hatua hiyo imewaweka katika ngumu wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, wakati ambapo vikwazo vya kisiasa na kiuchumi tayari vinachangia pakubwa kiwango cha ukosefu wa ajira ambacho kimefikia asilimia 60. Eneo hilo linakabiliwa pia na ukosefu wa nguvu za umeme ambapo mara nyingine umeme hukatika kwa muda wa saa 18 kwa siku.

Mahmoud Hamdan, mkuu wa muungano wa wafanyakazi katika sekta ya elimu kwenye shirika hilo la UNRWA, amesema kukatizwa ufadhili huo wa fedha kutazidisha hali kuwa mbaya na kutasababisha athari kubwa kwa vijana. Wakati huo huo, Israeli imelalamika kuwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa UNRWA linawapa hadhi maalum wakimbizi wa Kipalestina, na kwamba baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wanaunga mkono shughuli za kigaidi na pia wana mahusiano na kundi la Hamas.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/newscom/B. Greenblatt

Mkurugenzi anayesimamia uendeshaji wa UNRWA katika Ukanda wa Gaza, Mattias Schmale, amekanusha madai ya Israeli na ameonya juu ya kutokea hali mbaya kwa wakimbizi wa Palestina ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Bwana Schmale amesema wamekuwa wanapata pesa za kuwasaidia wakimbizi wa Palestina na wala hawana pesa za kuitumikia Hamas amesisitiza kwamba hakuna taarifa wala ushahidi wowote kwamba rasilimali wanazozipata zinachukuliwa na Hamas. Mkurugenzi huyo amesema wanazitumia fedha hizo kuendesha huduma kwa ajili ya wakimbizi milioni 1.3.

Marekani ndio ilitoa mchango mkubwa kwa UNRWA, wa kiasi cha dola milioni 364 mwaka uliopita wa 2017. Hata hivyo, mwaka huu, utawala wa Trump ulipunguza dola milioni 304 na kuahidi kutoa dola milioni 60 peke yake.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linatoa elimu, afya na misaada kwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina wanaoishi katika kambi 58 zinazotambuliwa katika eneo hilo.

Waziri wa ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman
Waziri wa ulinzi wa Israel Avigdor LiebermanPicha: Reuters/N. Elias

Wakati huo huo Israeli imerudia kuweka vikwazo vya mafuta kupitia mpaka wa Kerem Shalom unaotumika kuvusha bidhaa kati ya Israeli na Gaza. Waziri wa Ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman amesema Wapalestina wameanza tena kurusha mioto kwa kutumia mchanganyiko wa vilipuzi aina ya Molotov na hadi kufikia siku ya Jumatano mioto hiyo ilikuwa imerushwa mara saba kwenye eneo la mpaka wake na Gaza.

Waziri wa ulinzi wa Israel amesema bidhaa hiyo ya mafuta imezuiwa kwa muda usiojulikana. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahirisha safarim yake ya Colombia kutokana na hali katika Ukanda wa Gaza.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo