1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gachagua: Idara ya Ujasusi yaifelisha serikali ya Kenya

26 Juni 2024

Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua, amesema Idara ya Ujasusi wa kitaifa imefeli kumshauri rais ipasavyo, hali iliyosababisha maafa kutokea nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/4hY4O
Kenia Wahlkampf Kenya Kwanza Alliance Rigathi Gachagua
Picha: Press service William Ruto

Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua amemtolea wito mkuu wa intelijensia nchini mwake Nurdin Haji ajiuzulu na awajibishwe kutokana na maafa yaliyotokea nchini Kenya yaliyofungamana na maandamano ya kupinga muswada wa fedha wa mwaka 2024.

Kulingana na Gachagua idara ya ujasusi nchini Kenya haikumpa rais ushauri muafaka kwamba Wakenya hawakuutaka mswada huo wa fedha.

Soma pia: Ruto auondoa kabisa muswada wa fedha 2024

Katika hotuba yake aliyoitoa moja kwa moja kupitia Televisheni ya kitaifa, naibu rais huyo wa Kenya amesema vifo vya raia, uharibifu wa mali na hata uvamizi wa taasisi muhimu za serikali vingeepukika iwapo rais angelipata ushauri muafaka kutoka kwa idara ya intelijensia, aliyoielezea kuyumba huku akimtaka Nurdin Haji kuwajibika kwa kulifelisha taifa la kenya kwa kutofanya kazi yake ipasavyo. 

Vijana waombwa kuachana na Maandamano

Kenya Maandamano
Vijana wameombwa kutowaadhibu wabunge kufuatia misimamo waliyochukua dhidi ya Muswada wa Fedha 2024. Picha: James Wakibia/Sipa USA/picture alliance

Gachagua Ameongeza kuwa Rais Ruto anapaswa kuwa na Idara imara ya intelijensia pamoja na viongozi wa intelijensia wanaoweza kutathimini hali kwa haraka na kumfahamisha kile kinachoendelea nchini.  

Soma pia: Kenya yafanya tathimini ya hali baada ya Maandamano

Akiwa mjini Mombasa alikotoa hotuba hiyo, Gachagua amewaomba vijana kufutilia mbali maandamano yao kwa sababu tayari rais amewasikiliza na kufanya kile kilichohitajika kwa kuutupilia mbali muswada huo tete. 

Amewataka vijana hao kuokoa maisha, kuzuwia umwagikaji damu na kuzuwia uharibifu wa mali kwa kuachana na mipango yao hiyo ili kutoa nafasi kwa serikali kuwa na mazungumzo na vijana kupata suluhu ya kisiasa. 

Soma pia: Rais wa Kenya aapa kuchukua hatua kali dhidi ya maandamano ya vurugu

Amekiri kwamba serikali imewafelisha watu wake huku akitoa wito wa mpango wa kuzisaidia familia zilizoathirika kufuatia maandamano ya kuupinga muswada huo tata yaliyosababisha mauaji ya watu zaidi ya 20 huku wengine wengi wakijeruhiwa. 

Amewataka pia vijana kutowaadhibu wabunge kufuatia misimamo waliyochukua.