1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yasema inawatimua wapiganaji wa TPLF Amhara na Afar

22 Desemba 2021

Serikali ya Ethiopia imesema jeshi lake linaviondoa vikosi vya Tigray, TPLF, kutoka majimbo ya Amhara na Afar kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/44gfj
Äthiopien | Norden | Rebellen Tigray
Picha: S.Getu/DW

Serikali hiyo imepuzilia mbali taarifa ya TPLF kwamba vikosi vyake vinaondoka kwa hiari  ili kuruhusu mchakato wa amani kuanza. 

Msemaji wa serikali ya shirikisho nchini Ethiopia Billene Seyoum amewaambia waandishi wa habari kwamba katika wiki za hivi karibuni wanajeshi wa serikali pamoja na washirika wao, wamekuwa na mafanikio makubwa katika majimbo ya Amhara na Afar kwa kuchukua udhibiti kutoka mikononi mwa TPLF.

TPLF waudhibiti tena mji wa Lalibela

Billene ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na mapambano makali katika majuma yaliyopita. Pambano la karibuni zaidi likiwa ni kuwatimua wapiganaji wa TPLF kutoka jimbo la kaskazini Wollo Zone na kukomboa mji wake mkuu ambao ni wa kimkakati, Woldiya.

Kulingana na Billene, majeshi ya serikali ya shirikisho yanaendelea kuvitimua vikosi vya TPLF katika maeneo mbalimbali ya majimbo hayo mawili.

Mnamo siku ya Jumatatu, chama cha TPLF kinachodhibiti jimbo la Tigray na ambacho kimekuwa kikipigana na serikali ya shirikisho la Ethiopia, kilitangaza kuwa vikosi vyake vinajiondoa katika miji ya majimbo jirani ya Amhara na Afar kwa hiari.

Ethiopia yadai kuidhibiti miji miwili kutoka kwa waasi

Mkuu wa TPLF Debretsion Gebremichael pamoja na msemaji wa chama hicho Getachew Reda wakikutana na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika (01.11.2021) kutafuta suluhisho la mzozo wa Ethiopia.
Mkuu wa TPLF Debretsion Gebremichael pamoja na msemaji wa chama hicho Getachew Reda wakikutana na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika (01.11.2021) kutafuta suluhisho la mzozo wa Ethiopia.Picha: Privat

TPLF yataka Ethiopia na Eritrea kuwekewa vikwazo vya silaha

Kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael ameuandikia Umoja wa Mataifa barua, akitaka usitishwaji wa ndege za adui kupaa katika anga ya Tigray. Ametaka pia Ethiopia na mshirika wake Eritrea ziwekewe vikwazo vya silaha na Umoja wa Mataifa uweke mpango wa kuthibitisha ikiwa vikosi vya kigeni vimeondoka Tigray.

Billene alipoulizwa kutoa kauli kuhusu barua hiyo ya mkuu wa TPLF, alijibu bila kutoa maelezo Zaidi akisema hana hata uhakika kuhusu uhalali wa barua kama hiyo kwa Umoja wa Mataifa, na kwamba serikali ya Ethiopia inaichukulia TPLF kama kundi la kigaidi.

Maelfu ya raia wameuawa kufuatia vita hivyo ambavyo vimedumu kwa miezi 13 sasa. Takriban watu 400,000 pia wanakabiliwa na njaa katika jimbo la Tigray kutokana na machafuko hayo. Aidha watu milioni 9.4 kaskazini mwa Ethiopia wanahitaji misaada ya chakula kaskazini mwa Ethiopia.

Ukamataji wa Watigrinya

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya shirikisho imewakamata na kuwafunga maelfu ya watu, wengi wakiwa Watigrinya kwa tuhuma ya kukiunga mkono chama cha TPLF.

Siku ya Jumanne Abraha Desta ambaye ndiye kiongozi wa ngazi ya juu miongoni mwa Watigrinya waliokamatwa, alitangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba ameachiliwa huru.

Abiy ambaye kuingia kwake mamlakani mnamo mwaka 2018 kulimaliza takriban miongo mitatu ya utawala wa TPLF, anadai chama cha TPLF kinataka kung'ang'ania mamlaka ya serikali kuu. Madai ambayo viongozi wa Tigray wanakanusha.
Abiy ambaye kuingia kwake mamlakani mnamo mwaka 2018 kulimaliza takriban miongo mitatu ya utawala wa TPLF, anadai chama cha TPLF kinataka kung'ang'ania mamlaka ya serikali kuu. Madai ambayo viongozi wa Tigray wanakanusha.Picha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

Pande zote mbili kwenye mgogoro huo, TPLF na serikali ya shirikisho zinanyoosheana vidole vya lawama.

TPLF inamshutumu waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa kutaka kunyakua mamlaka na madaraka yote bila kuzingazia majimbo, madai ambayo Abiy amekanusha.

Majeshi ya Ethiopia yatuhumiwa kushambulia raia Tigray

Msemaji wa serikali Billene alipoulizwa kuhusu madai ya vyombo vya Habari vya Tigray Pamoja na madai ya msemaji wa TPLF kuhusu mashambulizi  ya angani yaliyofanywa na vikosi vya Ethiopia dhidi ya raia katika jimbo la Tigray katika siku mbili zilizopita, alijibu kwa kuyakanusha. Aliongeza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa dhidi ya kambi na maficho ya wanamgambo.

Msemaji wa TPLF Getachew Reda alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa watu 30 waliuawa kufuatia shambulizi la ndege zisizohitaji rubani dhidi ya gari la kubeba abiria katika mji wa Mlazart. Na kwamba shambulizi mengine kama hayo yalifanyika pia maeneo ya Maychew na Korem.

(RTRE)