1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yadai kuidhibiti miji miwili kutoka kwa waasi

Sylvia Mwehozi
7 Desemba 2021

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuidhibiti tena miji miwili ya kimkakati ya Dessie na Kombolcha, mwezi mmoja baada ya kushikiliwa na wapiganaji wa Tigray

https://p.dw.com/p/43ulb
Äthiopien Tigray-Krise | Armee
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Hatua hiyo ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa ushindi wa haraka katika uwanja wa vita unaotangazwa na vikosi tiifu vya waziri mkuu Abiy Ahmed. 

Idara ya mawasiliano ya serikali imesema katika tangazo la kupitia Twitter kwamba miji ya Dessie na Kombolcha imekombolewa na vikosi vya usalama vya pamoja, ambavyo pia vilichukua udhibiti wa miji kadhaa upande wa mashariki. Miji hiyo miwili ambayo inapatikana katika mkoa wa Amhara katika barabara kuu, karibu kilometa 400 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Addis Ababa, ilikuwa imedhibitiwa na wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Kushikiliwa kwake kuliibua wasiwasi kuwa TPLF na washirika wake, jeshi la ukombozi wa Oromo wangezidi kusogea na kuingia mjini Addis Ababa na kusababisha mataifa ya kigeni kuwatahadharisha raia wake kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo. Shirika la utangazaji la taifa la Ethiopia limemnukuu waziri mkuu Abiy akisema kwamba waasi "wameshindwa vibaya sana na hawakuweza kuhimili mashambulizi ya vikosi vya pamoja", akiongeza kuwa adui atashindwa na ushindi utaendelea kupatikana.

Waziri Mkuu Abiy aliamua kuungana na wanajeshi wake katika uwanja wa mapambano mwezi uliopita, baada ya wapiganaji wa Tigray kudai kuwa wanayashikilia maeneo makuu wakati wakizidi kusonga kuelekea mji mkuu wa Addis Ababa. Serikali yake ilidai wiki iliyopita kuwa jeshi lilidhibiti eneo la Lalibela, ambalo liliangukia mikononi mwa waasi mwezi Agosti na vilevile mji wa Shewa Robitambao upo kilometa 220 kutoka Addis Ababa kwa barabara.

Äthiopien | Premierminister nimmt an Offensive gegen Rebellentruppen Teil
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akijiunga na wanajeshi katika mapambanoPicha: Ethiopian Prime Minister's Office//AA/picture alliance

Msemaji wa TPLF Getachew Reda aliandika kupitia Twitter Jumatatu jioni kwamba vikosi vya waasi vimeondoka katika miji ikiwemo Kombolcha na Dessie "kama sehemu ya mkakati". Siku moja kabla kiongozi wake Debretsion Gebremichael alikanusha madai ya serikali kupata ushindi mkubwa, akisema waasi walikuwa wakifanya marekebisho ya kimkakati na hawajashindwa.

Wakati huohuo, nchi sita ikiwemo Marekani zimeelezea wasiwasi juu ya ripoti za ukamataji mkubwa wa Watigrinya kwa kuzingatia misingi ya ukabila kuhusiana na mgogoro wa Tigray uliodumu kwa mwaka mmoja sasa, na kuitaka serikali kukomesha vitendo vinavyotajwa kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Nchi hizo zimenukuu ripoti za tume ya haki za binadamu ya Ethiopia na kundi la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International juu ya kukamatwa kwa watu wengi wa kabila la Tigrinya, sambamba na padri wa kiorthodoksi, wazee na mama wenye watoto.

Nchi hizo zimeongeza kuwa "zina wasiwasi mkubwa" juu ya kuwekwa kizuizini kwa watu bila kufunguliwa mashtaka, na kuongeza kuwa tangazo la serikali la hali ya hatari la mwezi uliopita, "halitoi uhalali" wa watu kukamatwa kwa wingi.

Vyanzo: afp/reuters