1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

ECOWAS yakataa kipindi cha mpito cha miaka mitatu Niger

Admin.WagnerD22 Agosti 2023

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, imekataa pendekezo la utawala wa kijeshi nchini Niger la kuunda serikali ya mpito na kisha kubakia madarakani kwa muda wa miaka mitatu kabla ya kuitisha uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4VQRf
Ghana Symbolbild ECOWAS Fahnen
Bendera ya ECOWAS na za baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo.Picha: Nipah Dennis/AFP

Msimamo huo unazidisha hamkani bila ya kuwepo ishara ya kupatikana mwafaka wa haraka kuhusu mzozo wa Niger. 

Kamishna wa masuala ya Usalama na Amani wa Jumuiya ya ECOWAS, Abdel-Fatau Musah amesema pendekezo hilo la watawala wa kijeshi ni sawa na "mzaha" na kwamba viongozi wa kanda hiyo "kamwe hawatalikubali".

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Aljezeera, Musah, amesema ECOWAS inataka kurejeshwa utawala wa katiba nchini Niger na kwamba mpango wa kuivamia kijeshi nchi hiyo bado uko mezani.

Amesema msimamo wa taasisi hiyo ya kikanda wa kuwataka majenerali walioipindua serikali waondoke madarakani bado haujabadilika.

Amesisitiza kwamba matakwa ya ECOWAS ya kuachiwa bila masharti kwa rais Mohammed Bazoum na kurejeshwa madarakani kwa serikali ya kiraia bado hayajaondolewa. 

Mkuu wa utawala wa kijeshi aonya dhidi ya matumizi ya nguvu 

Kiongozi wa kijeshi wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani
Kiongozi wa kijeshi wa Niger, Jenerali Abdourahamane TianiPicha: Télé Sahel/AFP

Msimamo huo wa ECOWAS umetolewa kwa mara nyingine baada kiongozi wa kijeshi wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, kusema Jumamosi iliyopita kuwa majenerali wanalenga kubakia madarakani kwa miaka mitatu kabla ya kurejea kwa utawala wa kiraia.

Tangazo hilo alilitoa muda mfupi kupitia hotuba yake kwa taifa baada ya ujumbe wa kidiplomasia wa ECOWAS kuitembelea Niger kujaribu kuwashawishi watawala hao wa kijeshi kuaachia madaraka.

Alitumia hotuba hiyo kusema jeshi liko tayari kwa mazungumzo kuhusu mzozo unaoligubika taifa hilo tangu walipochukua madaraka mnamo Julai 26. Lakini alionya juu ya taathira kubwa zitakazotokea iwapo ECOWAS itaamua kutumia mabavu kuwaondoa mamlakani.

Jumuiya ya ECOWAS tayari imeidhinisha mpango wa kuunda kikosi cha kijeshi kitakachouwa tayari ktuumwa nchini Niger pindi juhudi za kidiplomasia zitashindwa kuwashawishi wanajeshi kuachia madaraka.

Serikali za kijeshi zapigana jeki katikati ya mzozo 

Jumuiya hiyo imefaadhishwa na kile imekitaja kuwa mwenendo wa majeshi kupindua serikali kwenye kanda ya Afrika Magharibi.

Symbolbild Hilfsorganisationen befürchten humanitäre Katastrophe im Niger
Licha ya vizuizi dhidi ya uhuru wa kawaida vilivyowekwa baada ya mapinduzi, wengi ya wakaazi wa mji mkuu wa Niger, Niamey wanaunga mkono utawala wa kijeshi.Picha: AFP/Getty Images

Hivi sasa mbali ya Niger, nchi nyingine tatu za Mali, Guinea na Burkina Faso zimo chini ya tawala za wanajeshi waliofanya mapinduzi. Mbili kati ya hizo ambazo ni Mali na Burkina Faso zimesema zinapinga uingiliaji kati kijeshi nchini Niger na litauzingatia kuwa tangazo la vita.

Katika hatua nyingine msafara wa malori 300 yaliyobeba bidhaa na mahitaji muhimu umewasili jana kwenye mji mkuu wa niger, Niamey kutoka nchini Burkina Faso.

Afisa Mkuu anayesimamia ushuru wa forodha kwenye mji huo Kanali Adamou Zaroumeye amesema bidhaa zilizowasili ni pamoja na mahindi, chumvi na mahitaji mengine ya nyumbani.

"Kwa muda mrefu hakuna malori yaliyoweza kufika hapa kupitia njia hii inayotoka Burkina Faso. Lakini kufuatia operesheni za usalama zilizofanywa kwenye ushoroba huu na majeshi ya Burkina Faso na Niger tumepokea msafara wa kwanza na tunatumai zaidi itawasili siku zinazokuja" amesema afisa huyo.

Shehena hiyo ya bidhaa ni sehemu ya msaada wa Burkina Faso kwa jirani yake Niger inayokabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyowekwa na ECOWAS.